“Usisikilize wanaokushindanisha kuwa wewe ni mkali kuliko fulani” – Tale amshauri Jay Meody

Tale anahisi uadui unaoanzishwa na mashabiki kuwagombanisha na kuwasindanisha wasanii kuhusu nani mkali kuliko nani kunawapoteza wasanii wengi, na kumtaka Melody kutotumbukia katika shimo hilo.

Muhtasari

• Pia alimhakikisha kumuunga mkono katika lolote atakalo kulifanya, akisema kwamba kwake milango ipo wazi kumkaribisha Melody wakati wowote.

Jay Melody
Jay Melody
Image: Facebook

Meneja wa muda mrefu wa Diamond Platnumz, Babu Tale amemshauri Jay Melody kutokubali kushindanishwa kimuziki na baadhi ya mashabiki kuwa yeye ni mkali kuliko msanii Fulani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Tale aiandika ujumbe mrefu akiweka picha ya albamu ya Melody – Therapy – na kusema kwamba amechukua muda wake kusikiliza ngoma zake nyingi pamoja na albamu hiyo nzima na kubaini kwamba kijana huyo kutokea Morogoro ana kipaji kikubwa.

Leo nimemka na Mwana wa Ukae na mdogo wangu sana @realjaymelody. Katika kipindi cha kazi zake za muziki nimepata kusikiliza nyimbo zake nyingi lakini kubwa zaidi nimesikiliza Album yake nzima, kwa hakika hakuna wimbo wa kupeleka mbele kwa maana zote zinamsukumo wa kusisikilizwa zaidi ya mara moja kisha unafuata nyingine,” Babu Tale alimuasa.

Alimtaka kutoyumbishwa kutoka katika njia kuu ya muziki, na kumtaka kushikilia alipo kwa sasa, akisema kwamba uadui unaoanzishwa na mashabiki kuwagombanisha na kuwasindanisha wasanii kuhusu nani mkali kuliko nani kunawapoteza wasanii wengi, na kumtaka Melody kutotumbukia katika shimo hilo.

“Mdogo wangu kazia hapohapo na shikilia vizuri kamba ya kukupeleka mbele, kubwa zaidi usikae ukasikiliza kelele za watu, ambazo zinaweza kukuweka kwenye mstari wa kushindanishwa kuwa wewe ni mkali sijui zaidi ya fulani. Jiambie mwenyewe kuwa mimi ni zaidi ya yeyote mbele ya Mungu na hapo utafika mbali katika safari yako,” Tale alitema lulu.

Kuhusu albamu hiyo iliyotoka wiki chache zilizopita, Tale alisema kwamba anaamini kabisa soko la kisasa la muziki limejikita katika kile ambacho Melody alikiwasilisha kwenye albamu yake.

Pia alimhakikisha kumuunga mkono katika lolote atakalo kulifanya, akisema kwamba kwake milango ipo wazi kumkaribisha Melody wakati wowote.

“Nakukaribisha ukihitaji lolote toka kwangu, milango iko wazi wakati wote. Naendelea kukuona mbali sana na watanzania wanatakiwa wajue kuwa Bongo Fleva kwa sasa inafuata mkondo wa wasilisho lako. Kaza Mwana wa ukae na ukae ukijua na mimi ni sehemu ya mashabiki wako,” Tale aliongeza.

Kwa upande wake, Melody alionesha kushangazwa kwake kubaini kwamba Tale amekuwa shabiki wake kimya kimya na kumshukuru kwa nasaha zake.

“Dah hii ni kubwa sana muheshimiwa. Asante sana kwa nasaha zako. Nitazifanyia kazi,lakini pia nimefurahi kujua kuwa wewe ni miongoni mwa mashabiki zangu🙏 Nashukuru pia kwa kunifungulia milango ya ushirikiano na nitaitumia hii nafasi vizuri,“ Melody alishukuru.