Zuchu akata mzizi wa fitina baina ya Diamond na Alikiba kuhusu namba moja trending

Katika kipindi cha wiki mbili, Diamond na Alikiba wamekuwa wakishindania nambari moja kwenye trending, kabla ya Zuchu kuibukia na kuwatengua wote kwa mpigo.

Muhtasari

• Diamond alianza kushikilia nambari moja kwenye trending na wimbo wake wa Mapoz akiwashirikisha Jay Melody na Mr Blue.

Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Alikiba amtupia bomu la moto Diamond kisa wimbo wa kura
Image: FACEBOOK, INSTAGRAM

Hatimaye msanii na mpenzi wa Diamond Platnumz amekuja kuumaliza ushindani kuhusu nani mfalme wa kushikilia nambari moja kwenye trending ya nyimbo baina ya Diamond na Alikiba.

Diamond na Alikiba katika kipindi cha wiki mbili zilizopita wamekuwa wakishindana kuhusu nambari moja kwenye trending ambapo nyimbo zao zimekuwa zikishindana kuzoa takwimu za kufurahisha katika majukwaa mbalimbali ya kutiririsha miziki kidijitali ukanda wa Afrika Mashariki.

Diamond alianza kushikilia nambari moja kwenye trending na wimbo wake wa Mapoz akiwashirikisha Jay Melody na Mr Blue.

Baada ya siku chache, Alikiba na Nandy walikuja na kolabo yao ya Dah ambayo ilitengua Mapoz kutoka kilele mwa trending na kushikilia namba moja kwa Zaidi ya siku kumi bila kudunguiwa na kibao kingine chochote.

Alikiba alianza kumtambia Diamond akisema kwamba hamwezi kimuziki kwani yeye na Nandy tu waliwaangusha wasanii watatu wa Mapoz kwa maana ya Diamond, Jay Melody na Mr Blue.

Hata hivyo, msanii Zuchu amekuja kuukata mzizi wa fitina baina ya wababe hao wawili baada ya wimbo wake wa Zawadi kuzipiga chini ngoma za Alikiba na Diamond kutoka nambari moja kwenye trending.

Kwa Zuchu kuwatoa wawili hao kwenye namba moja na kuishikilia yeye, ni maana kwamba ameshawanyamazisha wote na kwa upande mwingine ni tambo kwa Diamond ambaye atakuwa anasema msanii wake amemkomoa kutoka kwa tambo za kejeli za Alikiba kisa Dah.