"Ahsante Mungu kwa zawadi hii" Willy Paul anunua gari jipya lenye nambari za usajili 666

Alionekana akipiga picha kando na gari hilo aina ya Mercedes Benz lenye rangi ya njano.

Muhtasari

• Kwenu nyinyi mashabiki wangu walionipa nafasi ya pili. Asanteni. Ni kwa ukarimu wako ndio nipo hapa nilipo - Pozee.

Pozee anunua gari jipya aina ya Mercedes Benz
Pozee anunua gari jipya aina ya Mercedes Benz
Image: Screengrab, Instagram

Kwa mara nyingine msanii Willy Paul amejipata katika gumzo kali mitandaoni kwa utata uliozunguka gari lake jipya aina ya Mercedes Benz ambalo alizindua asubuhi ya Jumamosi.

Msanii huyo alipakia video fupi ikilionesha gari hilo la kifahari lenye rangi ya njano ambapo kwa mbaali wimbo wake na msanii Jovial ulisikika ukiimba.

Alimshukuru Mungu kwa zawadi hiyo na kusema kwamba ni matokeo na matunda mema kutokana na kazi yake safi kimuziki ambayo amekuwa akiifanya, haswa mwaka huu.

“Mungu alitenda tena!!! Atukuzwe Mungu aliye juu.. asante baba yangu kwa zawadi nyingine nzuri... Niliamua kujipa zawadi kwa kazi nzuri ambayo nimekuwa nikifanya.. kwa MAUDHUI SAFI ambayo nimekuwa nikitoa,” Willy Paul aliandika kwenye Instagram yake.

Aliapa kuendelea na moyo kama huo na kufanya kazi ya kupendeza na kukosha mioyo ya mashabiki wake kwani wao ndio walisimama naye na kumpa nafasi nyingine ya kung’aa baada ya safari yake ya muziki kutishiwa na madai ya Diana Marua kuwa aliwahi jaribu kumbaka.

“Ninakusudia kuendelea kuwa hivyo... na kwenu nyinyi mashabiki wangu walionipa nafasi ya pili. Asanteni. Ni kwa ukarimu wako ndio nipo hapa nilipo...” Pozee aliandika.

Hata hivyo, kilichowashangaza wengi na kuzua gumzo mitandaoni ni baada ya nambari ya usajili ya gari lile kuonekana ikiwa na 666 – nambari ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihusishwa na jamii ya kishirikina na ushetani ya Freemason na Illuminati.

Wengi walionekana kumtetea wakifutilia mbali uwezekano wa namba hizo kuwa na maana ya nguvu za gizani na kusema kwamba msanii huyo amekuwa akitia bidi sana kimuziki na kujinunulia gari la kifahari kama hilo anafaa kupewa hongera..