Maoni: Alikiba na Diamond waige mfano wa Ronaldo na Messi na kuzika tofauti zao

Kwa muda mrefu, Alikiba na Diamond wamejulikana kuwa katika mgogoro mkubwa wa uhasama wa kimuziki.

Muhtasari

• Alikiba ambaye si mzungumzaji sana hata hivyo hajawahi sikika wazi akizungumzia uhasama wake na Diamond.

Picha ya pamoja ya Messi na Ronaldo na ile iliyohaririwa kuwaonyesha Alikiba na Diamond
Picha ya pamoja ya Messi na Ronaldo na ile iliyohaririwa kuwaonyesha Alikiba na Diamond
Image: Instagram,Hisani

Baada ya picha ya pamoja ya Ronaldo na Messi kutajwa kuwa maarufu zaidi duniani kwa siku mbili zilizopita baada ya kupokea ufuatiliaji mkubwa mitandaoni, watu mbali mbali sasa wamekuwa wakiihariri picha hiyo na kuwaweka watu maarufu wanaowajua kuhasimiana.

Jumatatu klabu ya Fenerbahce ilihariri picha hiyo kwa kutumia taratibu ya Photoshop na kumuongeza kiungo mshambuliaji wao Enner Valencia kando yao kutuma ujumbe kuwa ni mtu wa tatu maarufu duniani. Hilo lilifanyika baada ya Valencia kuifungia Ecuador mabao mawili katika mechi ya ufunguzi ya mashindanio ya kombe la dunia dhidi ya wenyeji Qatar.

Majirani zetu kutoka Bongo Tanzania pia hawajaachwa nyuma kwani wamepiga hatua nyingine kwa kuihariri picha ile na kubadilisha sura za Ronaldo na Messi.

Katika mbadala wa sura hizo, waliweka sura za wasanii Alikiba na Diamond Platnumz wakishiriki mchezo wa chess kama njia moja ya kuzika tofauti zao.

Kwa muda mrefu, Alikiba na Diamond wamejulikana kuwa katika mgogoro mkubwa wa uhasama wa kimuziki kiasi kwamba hawawezi onana jicho kwa jicho wala kupikika kwenye jungu moja.

Wahariri wa picha hiyo walituma ujumbe kwa wasanii hao wa Bongo Fleva kuiga mfano wa Messi na Ronado na kuzika tofauti zao ili kuitumikia tasnia ya muziki kwa umoja kama ambavyo wachezaji hao walionesha kwa kuonesha umoja na ushirikiano kwa sababu ya mchezo wa kandanda.

Ingawa ugomvi wao unajulikana, Diamond aliwahi jitokeza wazi na kusema kwamba hata yeye haelewi ni kwa nini wanahasimiana na Alikiba.

Msanii huyo alituhumu vyombo vya habari kwa kupalilia ugomvi huo na hata kuendeleza dhana kwa zaidi ya miaka 10 kuwa wawili hao ni maadui wa tangu jadi wakati wote walikuwa chipukizi kimuziki.

Hata hivyo kwenye moja ya wimbo wake wa ‘Nawaza’ Diamond alitaja kuwa ugomvi wake na Alikiba ulisababishwa na mbwembwe za ujana wao kugombani ubabe wa ushabiki.

Alikiba ambaye si mzungumzaji sana hata hivyo hajawahi sikika wazi akizungumzia uhasama wake na Diamond.