Babymama wa Bahati, Yvette Obura afurahia mtoto wake Mueni kuibuka wa kwanza darasani

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema mtoto Mueni alimfanya kujivuni kwa kuwa namba moja katika mtihani wa gredi ya kwanza.

Muhtasari

• Bahati na Yvette licha ya kutengana miaka kadhaa iliyopita, wamekuwa na ushirikiano mwema katika kumlea mtoto huyo.

Yvette Obura na bintiye Mueni
Yvette Obura na bintiye Mueni
Image: Instagram

Mjasiriamali wa biashara ya nguo ambaye pia ni mzazi mwenza wa msanii Bahati Kioko, Yvette Obura ni mama mwenye furaha baada ya binti yake Mueni Bahati kuibuka wa kwanza katika mtihani wa darasa lao.

Yvette alipakia picha ya matokeo ya mtihani huo wa gredi 1 ambayo Mueni anasoma na kuonesha kuwa aliibuka kidedea jambo ambalo lilimsisimua kama mama ambaye siku zote anamtakia mema mtoto wake na kujihisi wa kujivunia pindi anapompa fahari kama hiyo.

“Tafakari ni nani aliibuka wa kwanza katika darasa lao, mtoto Mueni Bahati ananizidi kunifanya nijihisi fahari shuleni,” Yvette Obura alimwaga radhi yote kwenye ukurasa wake wa Instagram.

 Yvette Obura licha ya kupishana kimaelewano na mwanamuziki na mwanasiasa bahati Kioko, wamekuwa wakionesha mfano bora wa jinsi uzazi wa ushirikiano unaweza leta tija katika maisha ya mtoto.

Licha ya Bahati kuoa mwanamke mwingine, Diana Marua, Yvette muda wote amekuwa akionekana kuwa na ukaribu na familia hiyo na hata wakati mmoja alimwachia Marua mtoto Mueni kukaa naye, jambo ambalo limewafanya wapenzi hao kuwa mfano wa kuigwa na wengi.

Hivi majuzi, Bahati alipakia picha akiwa na Mueni na kumsifia huku akimuahidi kuwa siku zote atahakikisha anampa maisha anayostahili.

Bahati pia alisema kuwa atakuwa shabiki namba moja kwa kitu chochote ambacho mtoto huyo atakifanya kwani mapenzi yake kwa mwanawe hayawezi kukadiriwa kwa kipimo chochote duniani.

Kwako Binti Yangu wa Kwanza- Kuzaliwa. Nitakuwa hapa kwa ajili yako kila wakati. Daima nitakuwa Shabiki wako Mkuu. Nakupenda kwa moyo Wangu wote ❤ @Mueni_Bahati,” Bahati alimmiminia sifa bintiye.

Katika picha hiyo ambapo aliipakia Instagram, Bahati alionekana kutembea na bintiye Muneni huku wameshikana mikono wakicheka na kutabasamu kwa furaha.