Davido kufunga sherehe za kombe la dunia, wiki kadhaa baada ya kifo cha mwanawe

Za ndani ziliripoti kuwa Davido alikuwa mmoja wa wasanii waliotarajiwa kufungua kombe la dunia lakini hilo halingewezekana kutokana na kifo cha mwanawe.

Muhtasari

• Ifeanyi, mwanawe Davido alifariki siku chache kuelekea kombe la dunia na msanii huyo hajaonekana kadharani tangu hapo.

Davido kutumbuiza kombe la dunia kufunga
Davido kutumbuiza kombe la dunia kufunga
Image: Instagram

Staa wa Afropop kutoka Nigeria Davido anatarajiwa kutumbuiza katika tamasha la kufunga mashindano ya kombe la dunia mwishoni mwa wiki kesho huko Qatar.

Ikiwa atajitokeza na kutumbuiza, basi Hii itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa msanii Davido kuonekana hadharani  tangu kifo cha mwanawe wa kipekee Ifeanyi aliyefariki wiki kadhaa zilizopita kufuatia kile vtombo vya habari kutoka Nigeria viliripoti kuwa ni kuzama katika bwawa la kuogelea nyumbani kwao Lagos.

Habari za Davido kutumbuiza katika sherehe za kufunga kombe la dunia zilifichuliwa na rafiki yake mfanyibiashara kutoka Hong Kong kwa jina Stephen Hung.

Kumbuka kwamba nyota huyo wa muziki hapo awali alipewa kadi ya kutumbuiza kwa wimbo wa Kombe la Dunia kwenye sherehe ya ufunguzi lakini hakuweza tena kufanya hivyo baada ya kumpoteza mwanawe, Ifeanyi.

Kulingana na Hung, ana furaha sana kwamba Davido amethibitisha kuwa atakuwa kwenye hafla ya kufunga mashindano ya kandanda.

Aliandika: “Nimefurahi sana kaka yangu @davido alithibitisha kuwa atatumbuiza kwenye sherehe za kufunga Kombe la Dunia Qatar. Siwezi kungoja kumuona huko."

Watu kadhaa walifurahia habari hiyo huku wengine wakisema nafasi hiyo ya kufunga kombe la dunia itakuwa moja murwa kama kumfariji kwa kuondokewa na malaika wake na pia kumkaribisha kwenye muziki.

Tangu kifo cha mwanawe, Davido na mkewe Chioma wamekuwa nadra sana kuonekana mitandaoni huku vyanzo vya karibu vikisema kuwa bado wangali katika mfungo wa maombolezo ya kifo cha ghafla cha mwanawe.

Wiki kadhaa zilizopita blogu ya Mpasho iliripoti kuwa Davido na Chioma waliunga harusi ya kisiri wiki moja baada ya kifo cha Ifeanyi, katika kile kilichosemekana kama njia moja ya kumhakikishia mpenzi wake upendo wa kiwango cha juu licha ya kubaki bila uzao wat umbo lake.