Ndoto yangu ilikuwa kuwa mwanasiasa - Zuchu afunguka

Alisema kipindi yupo chuoni aliwahi safiri mataifa mengi kama kiongozi wa wanafunzi.

Muhtasari

• Alisema kipindi anasafiri mataifa mengi, aliona jinsi siasa komavu inafanywa kinyume na siasa za mataifa mengi ya Afrika.

Zuchu
Zuchu
Image: Instagram

Msanii Zuchu amezungumza taaluma ambayo angefuata kando ya kuwa mwanamuziki.

Zuchu anahisi kwamba kama asingekuwa mwanamuziki basi angekuwa mwanasiasa shupavu sana wa taifa la Tanzania.

Alisema kuwa kipindi yupo chuoni, alizungumza sana mataifa mengi kama kiongozi wa wanafunzi na kuona jinsi siasa za nje zimekomaa kuliko za mataifa mengi ya Afrika.

Kama nisingekuwa Mwanamuziki basi ningekuwa Mwanasiasa, wakati nasoma chuo nilichagua kuwa Mwanasiasa baada ya kuzunguka Nchi mbalimbali Duniani ikiwemo India, niliona Tanzania tupo nyuma sana kwenye maswala ya siasa,” Zuchu alinukuliwa akisema.

Mwanamuziki huyo ambaye amesainiwa chini ya lebo ya WCB Wasafi alisema kuwa alilazimika kuasi siasa na kukumbatia muziki kutokana na ushawishi mkubwa wa mama yake.

Ikumbukwe mamake Zuchu, Khadija Kopa ni mwanamuziki wa muda mrefu ambaye alitamba na nyimbo aina ya Taarab na katika mahojiano fulani Zuchu alinukuliwa akisema kuwa mamake alikuwa na mchango mkubwa kwake kupata mkataba WCB.

Kutokana na urafiki wa karibu wa Khadija Kopa na bosi wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz, alimuunganisha naye na hivyo ndivyo alipata nafasi ya kuandikishwa kwenye lebo hiyo miaka miwili iliyopita.

Zuchu alizimulia kuwa Diamond alikuwa na shoo Morogoro ambapo mamake alialikwa na akamtaka kuandamana naye. Alipofika kule ndio alimtambulisha na Diamond na akaambiwa kufanya nyimbo kadhaa ambazo zilikataliwa lakini ile ya Wana ambayo ndio ilimtoa mwaka 2020 ikawa ndio imekubaliwa na kumhakikishia mkataba.

Hivi majuzi Zuchu amekubali kuwa yeye na bosi wake Diamond Platnumz ni wapenzi na hivi karibuni wanatarajiwa kuweka vitu wazi kabisa.