Diamond azindua studio za redio nyumbani kwa Zuchu

Diamond aliahidi kuwainua wasanii kadhaa kutoka Zanzibar kadri siku zinavyokwenda.

Muhtasari

• Diamond alitoa shukrani za dhati kwa Bw Mwinyi kwa kukubali mwaliko na akampongeza kwa juhudi zake za kuwanyanyua vijana.

•Zuchu ni miongoni mwa wasanii tajika ambao asili yao ni visiwa vya Zanzibar

Diamond Platnumz na Mhe Hussein Mwinyi wakati wa uzinduzi wa Wasafi FM.
Image: INSTAGRAM// WASAFI MEDIA

Bozi wa WCB Diamond Platnumz hatimaye amezindua studio mpya za Wasafi FM katika visiwa vya Zanzibar, mashariki mwa Tanzania.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi alikuwa mgeni maalum katika hafla ya uzinduzi wa studio hizo ambayo ilifanyika  siku ya Jumanne asubuhi katika eneo la Migombani, Mnara wa Mbao.

Siku ya Jumatatu, Diamond alitoa shukrani za dhati kwa Bw Mwinyi kwa kukubali mwaliko na akampongeza kwa juhudi zake za kuwanyanyua vijana.

"Ni baraka ya Kipekee kupata Bahati ya kuzinduliwa studio zetu za Wasafi FM na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Asante Mhe Rais kwa kuendelea kuwanyanyua Vijana. Wazanzibari na Watanzania wote tunawakaribisha katika uzinduzi wa studio yetu ya Wasafi FM  Zanzibar Kesho Saa mbili asubuhi Mnara wa Mbao coconut," Diamond alisema chini ya bango la kutangaza hafla hiyo.

Mama Dangote, Zuchu, Mbosso, mtangazaji Juma Lokole ni baadhi tu ya watu wengine ambao waliandamana na Diamond katika uzinduzi wa studio hizo.

"Mhe rais tunakuhakikishia tutatangaza utajiri wetu wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na maeneo ya uwekezaji kwa watalii na pia fursa ambazo tunaamini kabisa Wazanzibar wanaweza kuzitumia kwa utaji unaofanyika," Diamond alisewa wakati wa uzinduzi wa studio za Wasafi FM.

Pia aliahidi kuwainua wasanii kadhaa kutoka Zanzibar kadri siku zinavyokwenda. Zuchu ni miongoni mwa wasanii tajika ambao asili yao ni visiwa vya Zanzibar. Mama yake, Khadija Kopa ni gwiji wa taarab.