Diamond Platnumz asherehekea Krismasi akiwa amelazwa hospitalini

Kulazwa kwake kunakujasiku moja baada ya kuahirisha tamasha lake nchini Burundi.

Muhtasari

• Mashabiki wake waifurika mitandaoni kumtakia kupona kwa haraka.

Msanii Platnumz akiwa hospitalini
Msanii Platnumz akiwa hospitalini
Image: INSTAGRAM

Mashabiki wa msanii namba moja wa muda wote ukanda wa Afrika Mashariki katika kitengo cha muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz wamejawa na wasiwasi baada ya msanii wao pendwa kupakia video kwenye instastory yake akiwa amelazwa hospitalini.

Diamond alipakia kipande hicho cha video kwenye Instagram yake na alionekana kuwa katika kitanda cha hospitali akiwa ametundikwa drip ya maji huku akifuatisha kwa maandishi ya mashaka kuwa huu ndio msimu wa krismasi mbaya sana katika maisha yake kwani amelazimika kusalia katika kitanda cha hospitali sikukuu ya Krismasi.

Katika vido hiyo, Diamond Platnumz alionekana mwenye maumivu makali huku akipata taabu sana kujipendua na kujisogeza. Kando ya kitanda cha hospitali paliponekana mama mmoja anayekisiwa kuwa mama Dangote akiwa ameweka mikono yake kwa nyuma kwa wasiwasi mno akimtizama mwanawe jinsi anajigaragaza kitandani kwa uchungu na maumivu.

Video hiyo pia inaendelea wakionekana matabibu na wauguzi wakijitahidi kwa hali na mali kumwekea drip za maji kwenye mkono wake.

Taarifa za Diamond kulazwa zinakuja siku chache tu baada yake kuahirisha tamasha lake ambalo lilikuwa linatarajiwa kufanyika nchini Burundi siku hiyo ya Krismasi katika kile wajumbe wake walisema ni maandalizi mabaya.

Mashabiki wake walifurika mitandaoni na kumtakia kheri njema na nafuu ya haraka huku wengine wakizusha kuwa huenda ni moja ya kiki zake za kila mara ambazo wamezoea kutoka kwake.

Msanii huyo siku moja nyuma kabla ya kulazwa alikuwa ameachia kibao chake kipya kwa jina Chitaki ambacho kinazidi kutekenya mitandao ya kijamii kwa kasi ya moto wa jangwani.