Fahamu kiasi kikubwa cha pesa ambacho Diamond analipwa kwenye show moja

Diamond anaaminika kuenda nyumbani na mamilioni baada ya kila shoo.

Muhtasari

•Kwa mujibu wa meneja wake Sallam SK Mendez, inagharimu shilingi milioni 230 za Kitanzania kumpata Diamond kutumbuiza nje ya Tanzania.

•Sallam alibainisha kuwa Diamond huwa anaalikwa kutumbuiza katika nchi nyingi za Afrika ambako anashabikiwa sana.

Diamond Platnumz
Image: Diamond Platnumz Instagram

Bila shaka, bosi wa WCB Diamond Platnumz ni mmoja kati ya wasanii wakubwa zaidi na wanaofuatiliwa sana barani Afrika.

Umaarufu na jina kubwa la staa huyo wa Bongo limemfanya kuwa miongoni mwa wasanii wa Kiafrika ghali zaidi kote duniani.

Diamond ambaye ametumbuiza katika majukwaa mengi ya kimataifa anaaminika kuenda nyumbani na mamilioni baada ya kila shoo.

Kwa mujibu wa meneja wake Sallam SK Mendez, inagharimu shilingi milioni 230 za Kitanzania kumpata Diamond kutumbuiza nje ya Tanzania.

"Analipwa kama milioni 230 nje ya Tanzania. Kimsingi imewekwa kiwango hicho," alisema katika mahojiano na kituo moja cha redio cha Bongo.

Shilingi milioni 230 za Kitanzania ni takriban shilingi milioni 12.1 za Kenya.

Mendez hata hivyo alidokeza kuwa msanii huyo  analipwa kiasi kidogo, ambacho hakijapangwa katika shoo zake za ndani ya Tanzania.

Meneja huyoalibainisha kuwa Diamond huwa anaalikwa kutumbuiza katika nchi nyingi za Afrika ambako anashabikiwa sana. Pia alidokeza kuwa wanaendelea kufanya mipango ya kuweza kupenya kwenye majukwaa ya Marekani na Uingereza ambako kufikia sasa imekuwa ni vigumu kwa wasanii wa Bongo kutumbuiza.

Ufichuzi wa Sallam unakuja siku chache tu baada ya mwimbaji wa Tanzania Master J kudai kwamba Diamond  huwa anatengeneza hela nyingi  zaidi kwa shoo moja kuliko wasanii wote wa Kenya wakiunganishwa.

“Mara ya mwisho nilipocheki Diamond anaingiza pesa nyingi kwenye show moja kuliko wasanii wenu wote wa A-list ukijumlisha. Au umesahau, una taarifa potofu,” alisema huku akimjibu mtumizi wa mitandao wa Kenya aliyesema wasanii wa Kenya wanapata pesa nyingi zaidi kuliko wenzao wa Bongo.

Takriban miezi minne iliyopita,  Diamond alidaiwa kuvuna takriban shilingi milioni 12 kutoka kwa shoo yake ya dakika chache katika uwanja wa Kasarani wakati wa mkutano wa siasa wa mwisho wa muungano wa Azimio-One Kenya.

Bosi huyo wa WCB ndiye aliyekuwa msanii mgeni maalum kwenye mkutano huo na alitua nchini kutumia ndege yake ya kibinafsi kisha kuchukuliwa na chopper ya Azimio hadi kwenye uwanja wa Kasarani.

"Azimio alilipia chopper yake tu, alilipwa milioni 12 na vigogo wa Tanzania kutumbuiza kwa dakika tatu," chanzo cha habari kilisema.

Diamond pia amewahi kufanya shoo zingine nchini Kenya ambazo anaripotiwa kulipwa mamilioni ya pesa.