Esther Musila asherehekea mwaka mmoja wa ndoa na Guradina Angel, "Kila siku ni fungate!"

"Mpenzi wangu, moyo wangu umejaa shukrani kwa upendo na urafiki unaotoka kwako" Musila alisema.

Muhtasari

• Ndoa ya wawili hao iligonga vichwa vya habari haswa kutokana na utofauti uliopo baina ya umri wa Guardian Angel mwenye miaka 31 na Musila mwenye miaka 53.

• "Safari hii imekuwa nzuri, mimi bado ni mchumba wako, wewe bado ni bwana harusi wangu." - Musila

Musila na Angel washerehekea mwaka mmoja wa ndoa
Musila na Angel washerehekea mwaka mmoja wa ndoa
Image: Instagram

Esther Musila, ambaye ni mke halali kabisa wa ndoa kwa mwanamuziki wa injili Guardian Angel amejawa na furaha akisherehekea mwaka mmoja tangu kufunga ndoa na mumewe.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Musila ameibua kumbukumbu kuwa mwaka jana Januari tarehe 4, tarehe sawa na leo, alisema ‘ndoa’ kwa ombi la Guardian Angel na kula yamini mbele ya umati mchache wa watu ambao walijitokeza kushuhudia tukio hilo ambalo ni la kupendeza machoni pa Mungu.

Musila alipakia picha za kipindi hicho akisema kuwa uamuzi wa maana kabisa alioufanya mwanzoni mwa mwaka 2022 ni kukubali kuolewa na rafiki yake wa karibu mno – Guardian Angel.

Alisema kuwa katika hadithi za kimapenzi zote duniani ambazo zitasimuliwa, basi yao itakuwa hadithi ya kuyeyusha moyo wake muda wote na siku zote.

“04.01.2022...Mwaka mmoja uliopita katika siku hii, nilifunga ndoa na rafiki yangu mkubwa na kati ya hadithi zote za mapenzi duniani, hadithi yetu itakuwa ni kipenzi changu daima. Safari hii imekuwa nzuri, mimi bado ni mchumba wako, wewe bado ni bwana harusi wangu. Mwaka mmoja umepita lakini bado ni kama fungate...” Musila aliandika.

Musila alimsifia mumewe Guardian Angel na kumtaja kuwa mwanaume anayejua thamani ya mapenzi na ambaye amefanya uhusiano wao kuwa rahisi kabisa kuendelea huku akimuahidi mapenzi yasiyojua ukomo.

“Kila siku nakupenda zaidi ya siku iliyopita. Unafanya Mr & Mrs kuonekane rahisi sana.... Heri ya kumbukumbu ya miaka mpendwa wa maisha yangu na mengine mengi yajayo.🥂🥂🥂 Nakupenda Bwana Omwaka,” Musila alisema.

Musila pia aliendelea mbele na kumuandikia Guardian Angel ujumbe mtamu akimshukuru kwa vicheko visivyo na mwisho mpaka usiku wa manane.

“Mpenzi wangu, moyo wangu umejaa shukrani kwa upendo na urafiki unaotoka kwako. Asante kwa vicheko vya usiku wa manane na busu za asubuhi unazoniogesha nazo. Asante kwa kunionyesha unyenyekevu na kuwa baraka kwa maisha yangu. Kila dakika ya maisha yangu na wewe imekuwa ya kukumbukwa,” alisema.

Ndoa ya wawili hao iligonga vichwa vya habari haswa kutokana na utofauti uliopo baina ya umri wa Guardian Angel mwenye miaka 31 na Musila mwenye miaka 53.