Penda anayekupenda jinsi ulivyo, maisha ni mafupi - Esther Musila ashauri

Musila na Angel walifunga ndoa yao iliyohudhuriwa na watu wa maribu mapema mwaka 2022.

Muhtasari

• Wawili hao wamekuwa wakisutwa kutokana na dhana ya upana wa umri baina yao.

• Esther Musila ana miaka 53 huku Guardian Angel akiwa na miaka 31 tu!

Wapenzi Guardian Angel na Esther Musila wakidekezana kwa mahaba
Wapenzi Guardian Angel na Esther Musila wakidekezana kwa mahaba
Image: Instagram

Mke wa mwanamuziki wa injili Guardian Angel, Esther Musila ametoa ushauri na wosia kwa watu ambao wanashangaa mbona uhusiano wao unadumu hali ya kuwa wa watu wengine kila muda ni matatizo bin shida.

Kulingana na Musila, siri pekee ya uhusiano wako kudumu ni kupendana na mtu ambaye mnashibana katika kila kitu maishani – kama yeye alivyompaka mwimbaji Guardian Angel na kushibana licha ya umri baina yao kuwa mpana kama mashariki na magharibi.

“Tafuta mtu ambaye anakupenda kwa jinsi ulivyo. Maisha ni mafupi!” Musila alisema huku mpenzi wake Guardian Angel akimdhihirisia upendo kwa kumwita malkia wa himaya yake.

Wiki chache zilizopita, Angel alipakia picha yake na Musila na kusema kuwa hata watupiwe maneno kutoka kila Pande, upendo wao haupo katika mkondo wa kuvunjika leo wala kesho kwani wanaobashiri hivyo tayari wameshabuma na kuchoma bet zao.

Alisema kuwa siku zote Musila atasalia kuwa ‘crush’ wake na hakuna siku atakaa aje kubadilisha mtazamo wake katika hilo, hata kwa dawa wala ulozi.

“Kile ambacho Mungu amenifanyia, huyu ndiye crush wangu wa milele,” Guardian Angel aliandika Instagram.

Ndoa yao iligonga vyombo vya habari na mablogu Afrika Mashariki kutokana na kwamba Guradian Angel ni mdogo zaidi kiumri kulinganishwa na Musila.

Guardian Angel ana miaka 31 huku Musila mkewe akiwa na miaka 53, tofauti ya miaka ishirini na ushee kati ya wapenzi hao.

Hivi majuzi mwanamuziki huyo alimsifia Musila na kusema kwamba tangu wajuane ameona mafanikio makubwa pamoja na mabadiliko katika maisha yake.

Ama kweli mapenzi yametaradadi!