Mrembo wa Harmonize Feza Kessy haambiliki wala hasemezeki, ajiita Feza Konde

Baadhi ya watu walimuonya kupungusa kasi ya mahaba yake kabla hajalia kama waliomtangulia ubavuni mwa Harmonize.

Muhtasari

• Harmonize alimuonesha mrembo huyo wiki jana, siku kadhaa tu baada ya fununu za kuachana na Kajala.

Harmonize na anayedaiwa kuwa mpenzi wake mpya Feza Kessy
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Mpenzi mpya wa msanii Harmonize, Feza Kessy ametahadharishwa na wengi dhidi ya kujiingiza zaidi kimapenzi na msanii huyo kutokana na rekodi yake ambayo imetajwa kuwa mbovu ndidi ya wapenzi wake wa awali.

Kessy ambaye alionekana kama vixen katika wimbo mpya wa Harmonzie ‘Wote’ alikuwa amejiita Feza Konde kwenye chapisho lake Instagram, jambo lililovutia ushauri kutoka kwa baadhi ambao kama walimhurumia vile.

Mtangazaji wa kituo cha Wasafi FM Diva thee Bawse alimuusia kukoma kujipa majina kama hayo yanayohusiana na Harmonize kwa sababu akiendekeza vitu akma hivyo mwisho wa siku penzi likikolea atabwagwa na kujichukia.

Kulingana na Diva, pengine mwanadada huyo mpenzi mpya wa Harmonize anajikosha kwa upya wa huba na kutafuta ufuatiliaji mkubwa kwenye mitandao lakini hajui kuwa ndio mwanzo anazama na kujinasua kutakuwa kibarua kigumu.

“Dada acha kujiongeza jina jipya ili kutafuta likes, comments na followers. Utakuja siku kulia kama wenzako, tunakuomba tu kuzingatia ushauri huu maana sisi tuko pale mbali tumekaa tunafuatilia showbiz,” Diva alitoa ya moyoni kwa Kessy kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Harmonize alionekana na mwanadada huyo kwa mara ya kwanza wiki jana saa chache kabla ya kutoa wimbo wake mpya na kudokeza kuwa ndiye mpenzi mpya wa kuliziba pengo lililoachwa na aliyekuwa meneja na mpenzi wake Fridah Kajala Masanja.

Mshikadau mwenza katika lebo ya Konde Music Worldwide, Jembe ni Jembe hapo Jumatatu katika mazungumzo na kituo chake cha Redio alisema kuwa ni kweli Harmonize na Kajala hawako pamoja tena huku pia akisisitiza kuwa katu haungi mkono suala la kuchanganya mapenzi na kazi

“Kwa sasa ninachoweza kudhibitisha ni kwamba Kajala si mmoja wa wanafamilia wa Konde na tunamheshimu kwa ushirikiano ambao alionesha kwetu kipindi anafanya kazi na sisi. Lakini  mimi siingi mkono suala la kuchanganya mapenzi na kazi japo pia kujihusisha kwake kimapenzi na Harmonize sidhani kama kulikuwa na madhara hasi sababu sijaona bado,” Jembe ni Jembe alisema.