Mulamwah alininunulia 'lunch' ya Ksh 500 tu ili kufanya collabo na mimi - Choffuri afunguka

Mchekeshaji huyo alisema kuwa kijijini hawakuwa wanajua kulipisha ili kufanya collabo.

Muhtasari

• Choffuri alisema kuwa mara ya kwanza Mulamwah alikataa kujihusisha naye kwa vile ucheshi wake ulikuwa kwa lugha ya Kiluhya.

Choffuri azungumzia mara ya kwanza kufanya collabo na Mulamwah
Choffuri azungumzia mara ya kwanza kufanya collabo na Mulamwah
Image: Facebook

Mchekeshaji maarufu kutoka mkoa wa Magharibi wa Kenya, Choffuri amefunguka kuhusu uhusiano wake na mchekeshaji mwenza Mulamwah.

Katika mazungumza na mwanablogu chipukizi Bella Itemere, Choffuri alielezea kwa mapana kiini cha kile kinatajwa kuwa ni ugomvi baina yake na Mulamwah kutokana na ukubwa wa wawili hao katika Sanaa ya burudani.

Alisema kuwa kwa wakati mmoja, alijaribu kumfuata Mulamwah ili kushirikiana naye katika kufanya video ya ucheshi lakini alikataliwa kwamba anazungumza kwa lugha ya Kibukusu, jambo ambalo alisema lilimuumiza moyo sana.

“Nimewahi wafuata wengi tushirikiane lakini walikataa kwa sababu naongea Kibukusu. Walisema wao ni wa kimataifa na mimi ni wa mtaani tu. Mulamwah mara ya kwanza alikataa kwa kusema kuwa mashabiki wake ni wa kimataifa na hawangeweza kusikia kile ninasema,” Choffuri alisema.

Choffuri alisema kuwa Mulamwah baadae aligundua kuwa ana mvuto wa aina yake na ndio akamfuata kumuomba collabo. Alisema kuwa kipindi hicho hakuwa anajua kulipisha ili kufanya collabo na mtu, kwa maana hiyo alimuitisha tu chakula cha mchana.

“Alinipeleka kwa hoteli fulani akanunua chakula cha kama shilingi 500 hivi, na ndio tukafanya collabo,” Choffuri alisema.

Mchekeshaji huyo aligusia kile kinachokwamisha Sanaa ya Waluhya kufanya vizuri na kupata sura ya kitaifa na kimataifa. Alisema kuwa wengi wa wasanii ambao ni wa mwanzo kutusua wamekataa kuwashika mikono wale wanaochipukia.

Vile vile, Choffuri alisema anaunga mkono kwa asilimia mia mswada wa mchekeshaji Eric Omondi kuhusu kampeni ya #Play75%KE  akisema kuwa ni vizuri kusukuma na kuinua vipaji vya mtaani kabla ya kuanza kukumbatia vipaji vya kimataifa ambavyo vimenolewa makali na wenyewe.

“Eric ako sawa, lazima tuanze kukubali wasanii wa mitaani kwanza, ili hata hao wasanii wa kimataifa wakija, wanafaa kujua kuwa si lazima msanii wa kigeni ndio anatumbuiza wa mwisho. Inafaa msanii wa huku mwenye shoo awe ndio amafunga kazi na kuzima taa.”

Choffuri ni mchekeshaji wa kwanza kutoka mkoa wa Magharibi ambaye alianzisha vichekesho kwa lugha ya Kiluhya na akapata mapokezi makubwa sana kutoka kwa mashabiki wake, wakiwemo wale ambao hawaelewi lugha hiyo ya jamii ya Mulembe.

Kwa sasa, anashirikiana na mpenzi wake katika kusukuma kazi zake za Sanaa.