Rayvanny atangaza kujitosa kwenye siasa kuwania ubunge

msanii huyo sasa anaingia kwenye orodha ya Professor Jay, MwanaFA na wengine.

Muhtasari

• Msanii huyo alisema kuwa kuingia kwake katika siasa kutakuwa ni kufanya kazi za wananchi.

Rayvanny ajitosa siasani
Rayvanny ajitosa siasani
Image: TikTok

Mwanamuziki kinara wa lebo ya Next Level Music Rayvanny amedokeza kuwa katika siku za usoni, atajaribu bahati yake katika karata ya siasa.

Msanii huyo alipakia klipu kwenye ukurasa wake wa Tiktok alipoonekana amepiga suti kali nyeusi huku akisindikizwa kwenda kwa gari lake na walinzi, kuchora taswira kama ile ambayo huonekana kwa waheshimiwa.

Palisikika mtu mmoja akimfanyia utani kwa kumuita mbunge wa Mbeya Mjini, jambo lililootesha tabasamu usoni mwa msanii huyo ambaye aliamua kupasua mbarika kuwa siku za usoni atatathmini kujibwaga katika siasa katika kile alisema kuwa ni kuwafanyia wananchi kazi.

“Mwaka elfu mbii na ishirini na ngapi unagombea ubunge wa Mbeya Mjini?” alisikika akimuuliza mtu mmoja.

“Eeh Mungu akijaalia muda wowote tu nitawania ili kuwafanyia wananchi kazi ili tuhudumie taifa,” Rayvanny alijibu kwa mbwembwe zote kama mwanasiasa stadi.

Iwapo atafanikisha tamko hilo lake, Rayvanny atakuwa anajiunga na orodha ndefu ya wasanii wa Bongo ambao waliwahi jaribu karata yao katika siasa.

Alianza mwanamuziki mkongwe Professor Jay kujiunga siasa ambapo aligombea na kushinda ubunge wa Mikumi na kisha katika uchaguzi uliopita Mwana FA aligombea ubungwe wa Muheza na kuibuka mshindi.

Jokate Mwegelo pia aliteuliwa kama DC na hayati rais Magufuli, wadhifa ambao ameushikilia mpaka hivi sasa.

Msanii Harmonize pia aliwahi dokeza nia ya kuwania ubunge wa kwao Mtwara haswa baada ya kupata ushawishi na msukumo mkubwa kutoka kwa Magufuli lakini ndoto yake kama vile ilididimizwa kufuatia kifo cha rais huyo na tangu hapo Harmonize hajasikika sana akizungumzia kuhusu siasa.