Trio Mio: Napanga kufanya collabo na Diamond, Zuchu na Nyashinski

Trio Mio pia alisema ndoto yake kuu ni kufanya collabo na rapa wa Uingereza, Central Cee.

Muhtasari

• Alimsifia sana rapa mkongwe Nyashinski akisema kuwa anatumai siku moja ataingia kwenye studio na yeye kufanya ngoma

Trio Mio kufanya ngoma na Diamond
Trio Mio kufanya ngoma na Diamond
Image: Instagram

Msanii Trio Mio siku tatu zilizopita aliachia collabo yake ya kwanza tangu sakata la matokeo ya mtihani wa KCSEmwezi mmoja uliopita.

Kibao hicho kwa jina Everyday alimshirikisha msanii mwenye uzoefu wa aina yake kutoka bendi ya Sauti Sol, Savara.

Baada ya ngoma hiyo kupata mapokezi mazuri kutoka kwa mashabiki zake, Trio Mio sasa ameorodhesha wasanii kadhaa ambao anataka kufanya collabo nao hivi karibuni, kwani sasa hana mambo mengine ya kuziwekeza fikira zake isipokuwa muziki.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, msanii huyo kinda alisema kuwa ana ndoto ya kufanya muziki na wasanii kadhaa ambao pia wanafanya vizuri katika muziki, wakiwemo wa humu nchini, wa mataifa jirani na wa kimataifa pia.

Alimsifia sana rapa mkongwe Nyashinski akisema kuwa anatumai siku moja ataingia kwenye studio na yeye kufanya ngoma. Pia alisema ndoto yake kuu ni kufanya collabo na rapa kutoka Uingereza, Central Cee, wasanii kutoka Tanzania kina Diamond Platnumz na msanii wake Zuchu miongoni mwa wengine.

“Kimataifa nimekuwa nikimfuatilia kwa muda mrefu rapa wa Uingereza Central Cee, Zuchu napenda sauti yake. Pia Diamond siwezi kata tunaweza tukatoa ngoma moto sana na yeye. Pia Nyashinski ningependa sana kufanya collabo nay eye siku moja,” Trio Mio aliweka bayana.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 18 mpaka sasa amepata ufanisi mkubwa katika tasnia ya muziki, akiwa amefanya collabo kadha wa kadha na wasanii kama vile Savara, Masauti, A-Pass, Ssaru miongoni mwa majina mengine makubwa katika muziki.