Diana Marua ataja sababu ya kutopakia picha za mtoto wa Yvette Obura, Mueni, chanzo mamake?

Marua alikuwa anazungumzia kutoonekana kwa mtoto wa Obura, Mueni pamoja na wenzake nyumbani kwake.

Muhtasari

• Mashabiki walikuwa wanauliza mbona Mueni siku hizi haonekani kwenye picha na video pamoja na wenzake kama awali.

• Marua alisema mamake Mueni, Yvette Obura ana chuki na hana shukrani.

Diana Marua asema Yvette obura ana chuki, mtu asiye na shukrani
Diana Marua asema Yvette obura ana chuki, mtu asiye na shukrani
Image: Instagram

Kwa muda mrefu mashabiki mitandaoni wamekuwa wakijiuliza uwepo wa mtoto wa Yvette Obura katika picha na video ambazo mke wa sasa wa Bahati, Diana Marua amekuwa akipakia.

Diana Marua katika siku za nyuma haswa kabla hajapata mtoto wa tatu, alikuwa akionekana anapakia picha za wanawe wote akiwemo Mueni, ambaye Bahati walizaa na mpenzi wake wa kwanza, Yvette Obura.

Lakini baada ya kujifungua mtoto Malaika, ghafla mashabiki wa wanandoa hao walianza kugundua uwepo wa Mueni kwenye familia ya Diana Marua na Bahati ulikuwa umeanza kufifia huku picha na video mitandaoni zikiwa ni za Marua, Bahati na watoto wao Morgan, Heaven, Majesty na mchanga Malaika.

Hilo limeendelea kushuhudiwa kwa miezi kadhaa sasa, baadhi wakihisi kwamba huenda kuna ufa uliotokea baina ya Yvette na Diana kumpelekea kumuondoa bintiwe kwenye familia ya rapa huyo.

Jumatano asubuhi, Diana kama kawaida yake alipakia video wanawe Morgan, Majesty na Heaven wakiondoka kwenye jumba lao la kifahari wakiwa ndani ya sare za shule tayari kuabiri gari la familia kwenda shuleni.

Mtumizi mmoja wa Instagram aliyefurahishwa na bashasha nyusoni mwa watoto hao alionesha kutoridhishwa kwake baada ya kukosa kumuona Mueni kwenye kikundi hicho ambacho alipenda kutangamana nao.

“Hebu tafakari kama Mueni alikuwepo pia😢 Vyovyote ilivyokuwa, ninakemea roho ya utengano kwa Jina la Yesu! Amani itawale na Mungu Amrudishe Mtoto Mueni nyumbani kwa ndugu zake,” mtumizi huyo kwa jina Damat Giriama aliandika.

Diana Marua ambaye amejaribu kukaa kimya kwa muda mrefu kuhusu sakala la kutoonekana tena kwa Mueni na wenzake, safari hii aliamua kutema ukweli wote.

Kwa njia ya mafumbo, Marua alidokeza kwamba kutoonekana kwa Mueni pamoja na wenzake chanzo ni mama yake – Yvette Obura. alisema kwamba huenda Obura alilazimika kuondoka na bintiye kutokana na chuki, kutokuwa na shukrani na kutema maneno makali ya matusi.

“Tusimshirikishe Yesu palipo na kutokuwa na shukrani, uchungu na chuki. Upendo na Nuru vitawale,” Diana Marua alijibu.

Ndio mwanzo mkoko unaalika maua, kaza mkanda na uchukue mkebe wako wa njugu mkononi!