Binti wa Sonko Sandra Mbuvi kujiunga kwenye siasa? "Nafuata nyayo za babangu!"

"Ninatazama kila hatua unayofanya, na ninajaribu kuchukua kila hatua unayochukua,” Sandra alimwambia babake.

Muhtasari

• Mrembo huyo alisema kila mara yupo karibu na baba yake licha ya kuwa mdogo lakini anahisi ujasiri wake unaongezeka.

Sandra Mbuvi adokeza kufuata nyayo za baba yake
Sandra Mbuvi adokeza kufuata nyayo za baba yake
Image: Instagram

Sandra Mbuvi, binti wa mfanyibiashara na mwanasiasa Mike Sonko amedokeza kwamba huenda wakati mmoja katika maisha yake akajitupa kwenye dimbwi la siasa.

Sandra alipakia picha wakiwa na baba yake na kusema kwamba anazifuata nyayo za baba yake kwa ukaribu mkubwa na kwamba anataka kuwa kama yeye katika kila kitu – ishara kwamba huenda atajaribu siasa pia.

Binti huyo ambaye juzi alisema hajawahi abiri gari la uchukuzi wa umma, matatu maisha yake yote alisema kwamba anajaribu kadri ya uwezo wake kufanya kila kitu kama ambavyo baba yake amekuwa akifanya.

“Katika mambo yote ninayojaribu kufanya, nataka kuyafanya kama wewe tu, ninatazama kila hatua unayofanya, na ninajaribu kuchukua kila hatua unayochukua,” Sandra alimwandikia baba yake Sonko.

Mrembo huyo alisema kuwa kila mara anapokuwa na baba yake licha ya kuwamdogo, lakini ujasiri wake unaongezeka akiwa kando ya baba yake.

“Ingawa mimi bado ni msichana wako mdogo, ninapokuwa na wewe ninahisi urefu wa futi kumi, kama wewe,” alisema.

Sonko alimjibu bintiye kwa makopakopa ya emoji za mapenzi ishara kwamba amekubali  matakwa na matarajio ya binti wake.

Awali, Sandra alidokeza kwamba hayuko kwenye soko la mapenzi sasa hivi kwani tayari ana mwanamume ila akasema wale wote wanaotarajia kumuona basi watasubiri sana kwa kuwa hayuko tayari kumuonesha kwenye mitandao ya kijamii.

Sandra alisema mwanamume kama hajamvisha pete ya uchumba, hawezi mpakia kwenye mitandao yake ya kijamii, na pia akasema hata ikatokea amemvisha pete, kupakia picha yake ni ngumu kwa sababu suala la mapenzi analichukulia kuwa la kibinafsi Zaidi.