Mke wa Samidoh amkimbilia Mungu ndoa yake ikiyumba, "Ee Mungu nikumbuke!"

Nderitu aliandika haya siku chache baada ya kudokeza ufa mkubwa katika ndoa yake na Samidoh.

Muhtasari

• Nderitu kwa miaka 3 sasa amekuwa akipigana vita vya kuimarisha ndoa yake dhidi ya Karen Nyamu ambaye amemgandia Samidoh.

Edday Nderitu arudi kwa Mungu ndoa yake ikiyumba
Edday Nderitu arudi kwa Mungu ndoa yake ikiyumba
Image: Facebook.

Edday Nderitu, mke wa mwanamuziki wa Mugithi Samidoh ambaye inasemekana wameachana ameandika ombi maalum kwa Mungu akitaka kukumbukwa.

Mama huyo wa watoto watatu alichapisha ombi hilo wiki moja baada ya kuandika ujumbe mrefu wenye ukakasi akidokeza kuwa amechoka na vitendo vya mume wake kutoka kimapenzi na seneta Karen Nyamu kwa muda wa miaka 3 iliyopita.

Nderitu sasa ameonekana kukubali na matokeo kuwa Samidoh hayuko karibu na kuachana na Nyamu licha ya kula yamini mara kadhaa kuwa hawezi tena kuonekana na seneta huyo asiyeweza kuepukika kutokana na mitego yake ya kimapenzi kwa Samidoh.

Mke wa kwanza wa Samidoh anaomba Mungu kumkumbuka kama alivyowakumbuka watu wengi katika simulizi za Biblia.

“Ee Mungu, nikumbuke. Nihurumie Bwana. Haya ndiyo maombi yenye nguvu zaidi ambayo daima hupata usikivu wa Mungu. Mungu akamkumbuka Sara, akafungua tumbo lake la uzazi. Mungu akamkumbuka Hana, akapata mimba. Mungu alimkumbuka Samson, nywele zake zilianza kukua. Huu ni wito wa huruma ya Mungu. Mungu akukumbuke wewe, watoto wako na Familia yako,” Nderitu alichapisha.

Ombi hili maalum kwa Mungu linakuja kipindi ambapo inakisiwa kuwa anapitia wakati mgumu sana, ikiwa kile alichokichapisha wiki moja iliyopita ni jambo la kuamini.

Nderitu alisema kwamba ndoa yake na Samidoh ambayo ina miaka 15 ilikuwa imeingiwa na msukosuko kutokana na mwanamuziki huyo kuchepuka mara kwa mara na mwanamke mmoja ambaye amekuwa donda sugu kwenye kiwiliwili chake – Karen Nyamu.

Alibainisha kwamba hakuwa tayari kuwalea watoto wake katika ndoa ya wanawake wawili na mke mwenza ambaye alimtaja kama mtu “asiye na adabu” jambo ambalo alisema kwa mara kadhaa ameliweka wazi machoni mwa mumewe Samidoh.

Lakini licha ya kunyoosha maelezo yote hayo, bado Samidoh amekuwa kama sikio la kufa ambalo kamwe halisikii dawa na kudokeza kuwa angetathmini kuiachia ndoa hiyo.