Wasanii waliotumbuiza Nairobi Festival mwezi Desemba walia kutolipwa hadi sasa!

Arrow Bwoy alizua kwamba amekuwa akiambiwa na wakala wa Homeboyz kuwa pesa bado hazijatoka kwa kaunti.

Muhtasari

• Wasanii hao walimtaka gavana Sakaja kuingilia kati na kutatua hilo kwani ni zaidi ya miezi 2 sasa na hawajapata malimbikizi yao.

Johnson Sakaja aombwa kuingilia kati malipo ya wasanii Nairobi Festival.
Johnson Sakaja aombwa kuingilia kati malipo ya wasanii Nairobi Festival.
Image: Facebook

Msanii wa kizazi kipya nchini Kenya, Arrow Bwoy amefichua kwa uchungu kwamba tangu kufanyika kwa tamasha la Nairobi Festival lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana, wasanii wote ambao walitumbuiza kwenye hafla hiyo wangali bado kulipwa.

Arrow Bwoy alimwandikia waraka gavana Sakaja ambaye alikuwa muasisi wa tamasha hilo akimtaka kutoa tamko lake kuhusu kutolipwa kwa wasanii hao kwa Zaidi ya miezi miwili sasa.

“Kwako gavana wetu mpendwa Sakaja, mambo yamechemka huku nje tangu tutumbuize katika tamasha la Nairobi Festival mnamo Desemba. Hatujalipwa,” Arrow Bwoy alisema.

Msanii huyo aliendelea kutoa maelezo Zaidi jinsi alipata mwaliko wa kuwa miongoni mwa makumi ya wasanii waliotumbuiza kwenye tamasha hilo lililofunguliwa na Sakaja wakati wa kuzindua rasmi bustani ya Uhuru kwa umma mnamo Desemba 12 baada ya sherehe za Jamhuri.

Arrow Bwoy alitafutwa na ajenti wa Homeboyz ambao walikuwa miongoni mwa wadhamini wa tamasha hilo lakini cha ajabu ni kwamba alipowaandikia kujua mbona malipo yake yamecheleweshwa, alipata jibu kuwa bado pesa hazijatolewa kutoka kwa uongozi wa kaunti ya Nairobi.

“Binafsi nilitafutwa na ajenti wa Homeboyz, uongozi wangu umejaribu kwa mara kadhaa kuwafikia ili kupata sababu ya kucheleweshwa kwa malipo yangu lakini, jibu lao ni kwamba pia hawajapokea pesa kutoka kwa kaunti…” Arrow Bwoy alilalama.

Tamasha la Nairobi Festival lilifanyika kwa takribani wiki moja katika bustani ya Uhuru, ambayo ilikuwa inafunguliwa rasmi kwa umma baada ya kufungwa kwa mwaka mmoja ili kupisha ukarabati.