Salasya ajumuika na Linet Toto kwa chakula, mwezi baada ya kutishia kumpachika mimba

Tangu Saasya kutamka maneno hayo yaliyotajwa kuwa ya dhihaka dhidi ya Toto, wawili hao wamekuwa wakionekana pamoja kwa nadra mno.

Muhtasari

• Mwezi mmoja uliopita, Salasya alijipata taabani baada ya makundi ya kina mama kumtaka kuomba radhi Toto kwa matamshi kuwa angemtunga mimba.

• Hata hivyo, Salasya alisimama kidete akisema hangeomba msamaha, lakini ni kama walisuluhisha tofuati zao kinyemela.

Wabunge Linet Toto na Peter Salasya wajumuika kwa chakula
Wabunge Linet Toto na Peter Salasya wajumuika kwa chakula
Image: Twitter

Hatimaye mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amekutana na mbunge wa kaunti ya Bomet Linet Toto katika mgahawa kwa chakula cha mchana.

Wabunge hao walikuwa wakijipatia chakula cha mchana kabla ya kufunga safari kwenda nchi jirani ya Tanzania kushiriki michezo ya wabunge wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika picha hiyo, Salasya ambaye alikuwa na tabasamu pana usoni alikuwa akila ugali huku Toto akiwa kando yake akiwa amevalia vazi jeusi.

“Na mheshimiwa Linet Toto na Mheshimiwa Charles Ngusya, Mbunge wa Mwingi Magharibi tukielekea Tanzania timu ya kenya ya riadha ya @NAssemblyKE miongoni mwa viongozi wengine,” Salasya aliandika kwenye picha hizo kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Hii ndio mara ya kwanza wawili hao wanaonekana hadharani tangu mwezi mmoja uliopita waligonga vichwa vya habari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa uhasama wa kisiasa baina yao.

Mwezi Februari, Salasya katika mkutano wa kinara wa Azimio Busia alipanda jukwaani akikashifu matamshi ya Toto kuhusu Odinga.

Salasya alitamka matamshi dhidi ya Toto ambayo makundi mengi yalisema ni kumdhalilisha mbunge huyo wa Bomet, aliposema kwamba alikuwa na nia ya kumtia mimba kama njia moja ya kumzima asiendelee kumshambulia Odinga.

“Kuna mwengine alichaguliwa kama hana pesa kama mimi, anaitwa Toto nitaenda kukaweka wiki kesho,” Salasya alisema.

Hili lilikuwa jibu kwa matamshi ya awali ya Toto katika hafla ya mbungwe wa Mogotio aliposema kwamba Odinga ni mzee aliyeanza siasa wakati hata yeye hakuwa amezaliwa, na kumtaka kutoendeleza upinzani dhidi ya serikali ya Ruto.

“Huyu mzee Raila Odinga alianza siasa zake za maandamano hata kabla sijazaliwa. Alianza siasa mwaka 1997 wakati sikuwa nimezaliwa na mpaka sasa bado anasema aliibiwa,” Linet Toto alisema.