Amber Ray aapa kupigana vikali dhidi ya Ex wanaomchafulia jina baada ya kuachana

Ray alitema moto huu baada ya Rapudo kuchapisha ujumbe wenye ukakasi kuwa huenda ujauzito huo si wake.

Muhtasari

• Baada yake kuweka wazi hilo, Rapudo kupitia ukurasa wake aliibua madai makali dhidi ya Ray, kuashiria kwamba huenda ndio sababu ya kuachana.

• Haijulikani kama ni ukweli au ni kiki kuwa wawili hao wameachana, japo kila mmoja ametoa taarifa yake kudhibitisha hilo kwenye kurasa zao.

Amber Ray atoa onyo kali dhidi ya ex wanaomchafulia jina baada ya kuachana.
Amber Ray atoa onyo kali dhidi ya ex wanaomchafulia jina baada ya kuachana.
Image: Instagram

Mwanasosholaiti Amber Ray ametangaza vita vikali dhidi ya wapenzi wake wa zamani ambao wana mazoea ya kumchafulia jina mitandaoni pindi baada ya kuachana.

Mrembo huyo ametoa tahadhari hii saa chache baada ya kudhibitisha kwamba uhusiano wake na Kennedy Rapudo umegonga mwamba.

Baada yake kuweka wazi hilo, Rapudo kupitia ukurasa wake aliibua madai makali dhidi ya Ray, kuashiria kwamba huenda ndio sababu ya kuachana.

Rapudo alionekana kuashiria kwamba huenda mtoto kijajo si wake, na kusema kwamba anasubiri hadi azaliwe miezi miwili ijayo ili kubainisha ukweli wote – matamshi ambayo hata hivyo aliyakanusha baadae.

Kufuatia hili, Ray ametangaza safari hii kusimama na kulipigania jina na haiba yake, kitu ambacho hakuwa anakifanya baada ya kuvunjika kwa mahusiano ya nyuma ambapo wapenzi wake aghalabu humchafulia jina kwa tuhuma na lawama nyingi.

“Kuna hii tabia ya watu wakitoka katika maisha yangu, wanaanza kuniharibia jina na huwa ninanyamaza kimya na siri zao hadi sasa hivi. Lakini sasa nimechoka. Mtu yeyote awe mpenzi wangu wa zamani au rafiki yangu wa zamani atanivaa, wewe jua mimi niko tayari kwenda kuzimu na kurudi kwa ajili ya kupambana nawe, safari hii nitapigana vita vya kujitetea,” Amber Ray alisema.

Awali, Ray aliweka wazi kwamba amemalizana kabisa na suala la mapenzi, akijiita mama asiye na mume, kwa watoto wawili – kwa maana ya mtoto wake wa kwanza na yule angali bado kuzaliwa.

Hata hivyo, wengi wa wafuasi wake Instagram wanahisi ni kiki wanafukuzia kwani hii si mara ya kwanza wanadokeza kuachana na Rapudo lakini baadae tena wanarudiana.

Wiki tatu zilizopita kabla ya kutanya dhihirisho ghali la kutangaza jinsia ya mwanao, wawili hao walikuwa wamefuta picha za kila mmoja Instagram, jambo lililozua uvumi kuwa wameachana.