DJ Fatxo akemewa vikali baada ya kusema anamuombea MC Fullstop ambaye pafu limefeli

Fullstop baada ya kudai kuwa pafu lake limefeli, Fatxo alimtia moyo na kumwambia kwamba anaendelea kumuombea usiku na mchana.

Muhtasari

• Hata hivyo, matamshi ya Fatxo kwamba anamuombea Fullstop yaliibua na kufufua tena wito wa kiharakati wa #JusticeForJeff.

Fatxo taabani kwa kusema anamuombea MC Fullstop
Fatxo taabani kwa kusema anamuombea MC Fullstop
Image: instagrm

Msanii wa muziki wa Kikuyu Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo amekosolewa vikali baada ya kujitolea kumuombea MC Fullstop (jina halisi John Maina) anayeugua.

Fullstop alishiriki chapisho la kuhuzunisha moyo kwenye mitandao ya kijamii ambapo alifichua kuwa pafu lake moja lilifeli kutokana na maambukizi ya Kifua Kikuu.

"Hii imeenda" kinadharia. Pafu langu la kushoto limefeli kabisa nimebaki na moja. Mnamo 2021 nilipatikana na TB ya mapafu ikaathiri mapafu kabisa," MC huyo wa reggae alisimulia Jumatano.

Alidokeza kutundika daruga katika tasnia ya burudani baada ya kufichua kuwa sauti yake pia imeathiriwa na TB.

"2022 nikapata TB ya koo nayo ikanimaliza sauti, Kukimbia, kutembea, kuongea ni shida. Alafu halafu mapafu yanameangusha, hayawezi jiponya kama ini. Itabidi nijipange hapa ninaona nikitundika daruga,” MC Fullstop alifafanua.

Miongoni mwa wasanii wa humu nchini ambao walitoa maneno ya kumtia moyo mtumbuizaji huyo ambaye ni mgonjwa ni pamoja na DJ Fatxo ambaye amekuwa akiangaziwa kufuatia kifo cha kutatanisha cha mjasiriamali Jeff Mwathi nyumbani kwake Kasarani.

"Oh Hapana!!! Usifikirie hata Kutundika buti kaka. Kuna Mungu Mbinguni Atakurejesha na Kuifufua Afya yako. Uko katika maombi yangu," Fatxo alisema.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walimkosoa msanii huyo huku wakionekana kufufua harakati ya #justiceforjeff.

Msanii Fatxo anazidi kuandamwa na upinzani mkali kutoka kwa mashabiki wake mitandaoni kufuatia kuhusishwa pakubwa na kifo cha kijana Jeff aliyefariki katika nyumba yake mapema mwezi Februari.

Ijumaa asubuhi, idara ya Upelelezi wa jinai DCI ilifanikiwa kuufufua mwili wa Mwathi kama hatua mwafaka ya kuendeleza uchunguzi wa kifo chake tata.