Akothee alinilipa milioni 1.4 kuwa MC katika harusi yake - Dr Ofweneke

Ofweneke alisema kuwa bei yake ya kuwa MC ilipanda mara dufu tangu kuwa mshereheshaji katika harusi ya Akothee.

Muhtasari

• "Nimemuona katika hali mbali mbali akiwa amefilisika, akiwa amefurahi. Na kumuona akifunga harusi ni kitu kizuri Zaidi" - Ofweneke.

Dr Ofweneke asema Akothee alimpa 1.4m kuwa MC wa harusi yake.
Dr Ofweneke asema Akothee alimpa 1.4m kuwa MC wa harusi yake.
Image: Instagram

Mchekeshaji ambaye pia ni mshereheshaji Dr Ofweneke kwa mara ya kwanza amefichua kiasi alicholipwa na Akothee ili kusherehesha kwenye harusi yake mapema Jumatatu wiki jana.

Akizungumza katika chaneli ya YouTube ya Presenter Ali, Ofweneke ambaye pia ni mtangazaji wa redio na runinga alisema kuwa Akothee ni rafiki yake wa karibu sana huku akifichua kiasi kikubwa alicholipwa kwa siku hiyo tu kwa ajili ya kuwa kama MC wa harusi kubwa ambayo imekuwa gumzo la miji na vijiji kwa wiki nzima.

“Sasa hivi bei yangu imepanda sana tangu Jumatatu. Akothee alinilipa milioni 1.4. Akothee ni rafiki wangu wa karibu sana. Nimemuona katika hali mbali mbali akiwa amefilisika, akiwa amefurahi. Na kumuona akifunga harusi ni kitu kizuri Zaidi ambacho ningekiona hata kama singekuwa MC pale,” Dr Ofweneke alisema.

Ofweneke alisema kuwa Akothee ni himizo kubwa sana kwa watoto wa kike kwamba ukiwa wewe kama wewe na uhalisia bila kufeki maisha, kila kitu kitanyooka tu upande wako kwa wakati wake.

“Mimi namkubali kwa sababu yule ni kama mimi tu ila kwa jinsia ya kike. Huwezi ukanichezea au kuzua mzaha kuhusu mambo yangu na ni kitu ambacho kinajulikana, kwa Akothee pia ni hivyo. Mimi nina furaha kwamba alipanda upendo. Na hi himizo kwa kina dada wote pale nje, mtapata upendo,” Dr Ofweneke alisema.

Jumatatu wiki jana, Akothee alifunga ndoa na mpenzi wake mzungu Denis Schweizer aliyembandika jina Omosh, arusi ambayo imeteka anga mitandaoni kote kwa wiki moja sasa.

Awali Radio Jambo tuliripoti kuwa Akothee ni himizo kubwa na amevunja ‘laana’ ya watu kwamba mwanamke wa Zaidi ya umri wa miaka 40 akiwa na watoto watano hawezi pata ndoa na kutulia.

Mbunge wa Mbita Milly Odhiambo pia alimpongeza na kusema hatua yake ya kufunga ndoa kwa mara ya pili ni mwanzo mpya kwa kina dada wote kuwa chochote kinawezekana na kufunga ndoa ya pili baada ya ile ya kwanza kubuma ni jambo linalowezekana bila tatizo.