Dadake Akothee, Cebbie Koks azungumza baada ya kukosa kuhudhuria harusi yake

Akothee alikuwa amedokeza kwamba amewaalika wote wanaohusika kwenye harusi hiyo yake ya pili.

Muhtasari

•Harusi ya pili ya Akothee ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii na wanasiasa mashuhuri nchini.

•Cebbie amesema anafahamu wanablogu wanamngoja atoe maoni kuhusu harusi hiyo na aeleze kwa nini hakuhudhuria. 

katika picha ya maktaba.
Cebbie Koks na dadake mkubwa Akothee katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM//

MCA wa kuteuliwa Elseba Awuor Kokeyo almaarufu Cebbie Koks Nyasego amezungumza baada ya kukosa kuhudhuria harusi ya dada yake mkubwa Esther Akoth almaarufu Akothee siku ya Jumatatu, Aprili 10.

Akothee na mumewe Denis Shweizer 'Omosh' walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi siku ya Jumatatu. Harusi hiyo ambayo ilikuwa ya pili ya mwimbaji huyo ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300  walikuwa wamealikwa kwenye hafla hiyo ya kufana.

Wakenya walikuwa wepesi kugundua kwamba dada mdogo wa mama huyo wa watoto watano, Cebbie Koks hakuonekana kwenye hafla hiyo huku baadhi wakielewa hali yake wakati wengine wakimkosoa kwa kutojitokeza.

Cebbie amesema anafahamu wanablogu wanamngoja kwa hamu atoe maoni kuhusu harusi hiyo na aeleze kwa nini hakuhudhuria. Hata hivyo amedokeza kwamba ataendelea kuwa kimya kuhusu hilo hadi milele.

Alitumia meme maarufu ya jamaa anayeonekana kusubiri kitu kwa hamu sana na juu yake akaandika, "Jinsi blogu zinangojea niseme neno ili waweze kuliunda tena ili liweze kueleza masimulizi yao huku wakiandika "Cebbie Koks avunja ukimya kwa ujumbe wa siri. ".. mtangoja sana nyinyi blogs."

Ujumbe huo unaonekana kuwafahamisha wanablogu kwamba hakutakuwa na 'chai' kutoka kwake baada ya kukosa harusi ya dadake. Kwa kweli, Wakenya wengi wamekuwa wakisubiri azungumzie hilo.

Kabla ya harusi, Akothee alikuwa amedokeza kwamba amewaalika wote wanaohusika kwenye harusi  hiyo yake ya pili.

Akihutubia wanahabari baada ya kutua kutoka Ufaransa, mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa ni wanawe wawili pekee, Prince Ojwang na Prince Oyoo ambao hawangefanikiwa kufika kwenye harusi hiyo kutokana na shule lakini akadokeza watashuhudia sherehe ya pili itakayofanyika Uswizi mnamo Julai 10.

"Karibu Prudence Vanpelt, bintiye Akothee. Msilete propaganda na siasa za familia kwa harusi yangu. Watu pekee ambao watakosa harusi yangu ni wanangu wawili ambao hawatafanikiwa kwa sababu ya sheria za shule, lakini watashuhudia ambayo imeratibiwa kufanyika Julai 10. Mwaka mzima Akothee anaolewa," alisema.

Mwezi Oktoba, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alifunguka kuhusu ugomvi wake na Cebbie na kutangaza hatakuwa akihudhuria hafla zake na vilevile watu wasitarajie kumuona  dadake huyo katika hafla yake.