Akothee adokeza kumwalika dadake mdogo kwenye harusi yake licha ya ugomvi wao

Mwanamuziki huyo alisusia kimakusudi harusi ya Cebbie Koks iliyofanyika Desemba mwaka jana.

Muhtasari

•Akothee aliweka wazi kuwa ni wanawe wawili pekee, Prince Ojwang na Prince Oyoo  ambao hawatafanikiwa kufika kwenye harusi hiyo.

•Mwaka jana, Akothee alitangaza kuwa hatakuwa akihudhuria hafla za Cebbie na vilevile watu wasitarajie kumuona katika hafla yake.

katika picha ya maktaba.
Cebbie Koks na dadake mkubwa Akothee katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM//

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amewasihi Wakenya kutoingiza siasa za familia katika harusi yake itakayofanyika tarehe 10 mwezi huu wa Aprili.

Akizungumza Jumamosi baada ya kumlaki nchini bintiye Fancy Makadia kutoka Ufaransa, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa ni wanawe wawili pekee, Prince Ojwang na Prince Oyoo  ambao hawatafanikiwa kufika kwenye harusi hiyo.

Alisema wanawe hao wawili wanaoishi Ufaransa hawatafanikiwa kwenye harusi yake ya pili kutokana na shule lakini akadokeza watashuhudia sherehe ya pili iliyoratibiwa kufanyika  nchini Uswizi mnamo Julai 10.

"Karibu Prudence Vanpelt, bintiye Akothee. Msilete propaganda na siasa za familia kwa harusi yangu. Watu pekee ambao watakosa harusi yangu ni wanangu wawili ambao hawatafanikiwa kwa sababu ya sheria za shule, lakini watashuhudia ambayo imeratibiwa kufanyika Julai 10. Mwaka mzima Akothee anaolewa," alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alifichua kwamba watu walioalikwa kupitia kadi ndio pekee watakaohudhuria harusi ya Jumatatu.

Kauli ya hivi punde ya mwanamuziki huyo inaonekana kujibu swali tata kuhusu iwapo dada yake mdogo, Cebbie Nyakokeyo atahudhuria harusi hiyo iliyotangazwa sana. Wawili hao wamekuwa wakizozana kwa muda huku Akothee hata akisusia harusi ya mdogo huyo wake  iliyofanyika Desemba mwaka jana.

Mwezi Oktoba, mama huyo wa watoto watano alifunguka kuhusu ugomvi wake na Cebbie na kutangaza kuwa hatakuwa akihudhuria hafla zake na vilevile watu wasitarajie kumuona  dadake huyo katika hafla yake.

Akothee alidai kuwa ugomvi kati yake na mdogo wake ulizidi kuwa mkubwa kwa kuwa mara nyingi familia yake ilikosa kuingilia kati.

"Mambo yalitua kwenye meza yangu ambayo yalinivunja lakini hayakuniua🙏 ,tena hakuna mtu aliyenyoosha mkono , nilibaki kupambana peke yangu. Tena kama mkubwa wao mambo yalilazimishwa kwenye koo yangu. Nilikubali kuwa mkubwa hadi nilipopunguzwa kuwa mkeka wa mlangoni," alisema.

Mama huyo wa watoto watano alifichua kwamba alivunjika moyo zaidi wakati dadake mdogo alipodai kuwa anajifanya  katika kipindi ambacho alikuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa takriban miezi sita.

"Niliporudi kwenye fahamu zangu, niliona ni vigumu kukubali ulikuwa mzaha, dada yangu hajawahi kunitembelea katika hospitali yoyote, si kwa njia mbaya lakini lazima alisafiri au kitu kama hicho, simlaumu,"

Alifichua kuwa wakati alipokuwa amelazwa hospitalini alimwandikia dadake barua akimueleza kwa nini lazima angejitenga naye.

Hata hivyo hakutuma barua hiyo hadi tarehe 31 Desemba 2021  kwa kuwa kila siku alitumai wangeweza kuzika uhasama wao. Alifichua kuwa alimblock dadake baada ya kupata ujasiri wa kutuma barua aliyokuwa amehifadhi kwa muda

"Nilisubiri dada yangu aje aseme (dada , unajua nini , samahani kwa maumivu yote niliyosababisha, tuzike yaliyopita na tujikusanye🙏) Hapana, familia iliendelea kusisitiza niwe wa kwanza kuenda kwake. Niliumia na kuumia, kwani sio mimi niliyesababisha tofauti, sio ile ninayoijua," alisema.

"Kweli, najivunia sana dada yangu, kutoka chini ya moyo wangu. Ninamtakia maisha bora zaidi, maisha yake ya baadaye yawe safi kama nyota. Nimemsamehe hadharani dada yangu, yuko na bado atabaki kuwa DAMU yangu."