Akothee afichua hatua kali alizochukua baada ya kupambana na msongo wa mawazo mara 5

Mwimbaji huyo alisema alikumbwa na msongo wa mawazo mwaka wa 2018, 2019 na 2021.

Muhtasari

•Akothee aliweka wazi kwamba, ingawa hali hiyo haikumbadilisha, mambo kadhaa katika maisha yake yalibadilika kutokana na masomo ambayo alijifunza wakati huo.

•Amefichua baada ya kupambana na hali hiyo aliweka mipaka ili kulinda afya yake ya akili na kuepuka kujipata pale tena.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua kwamba alipambana na msongo wa mawazo mara tano kati ya mwaka wa 2018 na 2021.

Siku ya Jumatano asubuhi, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kwamba, ingawa hali hiyo haikumbadilisha, mambo kadhaa katika maisha yake yalibadilika kutokana na masomo ambayo alijifunza wakati huo.

“Sijabadilika, nyote mlinionyesha nyinyi ni nani, niliwapa kilicho bora zaidi, hicho ndicho ambacho ningeweza kutoa, endapo ningeendelea zaidi ya hapo, ningejikuta katika hali hii (msongo wa mawazo), mitaani au futi 6 chini," alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kwamba alikumbwa na msongo wa mawazo mwaka wa 2018, 2019 na 2021.

Amefichua baada ya kupambana na hali hiyo aliweka mipaka ili kulinda afya yake ya akili na kuepuka kujipata pale tena.

"Nilijenga mipaka ili kulinda utimamu wangu. Baada ya kupambana na msongo wa mawazo bila kujua, sasa ninalinda nafasi yangu kama ni maisha na kifo," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Miongoni mwa hatua alizochukua ni pamoja na: 

1. Kuachilia chochote kinachoharibu amani yake.

2. Kuepuka kuahirisha mambo na kufanya yaliyo sawa kwa wakati unaofaa.

3. Kusema HAPANA kwa yasiyompendeza.

4. Kuondoka kwenye vikundi vya WhatsApp mara moja baada ya kuhisi mazingira yake yameanza kuwa sumu.

5. Kuepuka siasa za familia kadri awezavyo.

6. Kuzuia tetesi kabla hazijamuingia.

7. Kuepuka majibizano kwenye mitandao ya kijamii.

 8. Kuachilia watu wenye uhusiano hasi karibu naye na kuwaambia.

9. Kujitenga na marafiki na wanaompigia kelele au kufanya kama anawahitaji zaidi ya wanavyomhitaji.

10.Kublock watu, kunyima watu pesa kama hajiskii kuwapa.

 11 Kufanya tu jambo lililo sawa kwa wakati ufaao, pamoja na watu wanaofaa.