"Wanamuita Dennis" Akothee afichua sababu ya watoto wake kutomtambua mpenziwe kama baba

Kwa mzaha alisema kuwa binti zake wanapaswa kuwaita waume zao 'baba'.

Muhtasari

•Akothee alibainisha kwamba mpenzi wake huyo mzungu anaelewa jinsi ya kuhusiana vizuri na watoto wake wote.

•Akothee alisema watoto wake huwa wanamuita mpenziwe kwa jina lake halisi  kwani tayari wamekomaa kiumri.

Akothee na mabinti zake
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasirimali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua kwamba kuna uhusiano mzuri kabisa baina ya watoto wake watano na mchumba wake anayepanga harusi naye, Bw Omosh.

Akizungumza na wanahabari katika uwanja wa ndege wa JKIA baada ya kuwasili Kenya kutoka Ulaya siku ya Alhamisi, alibainisha kuwa mpenziwe huyo mzungu anaelewa jinsi ya kuwasiliana vizuri na watoto wake.

"Watoto wangu wanampenda, wanampenda sana. Omosh anatoboka. Anajua jinsi ya kushughulikia watoto wangu," alisema.

Hata hivyo, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alifichua kwamba watoto wake huwa hawamuiti mpenziwe 'baba'.

Aliweka wazi kwamba huwa wanamuita kwa jina lake halisi  kwani tayari wamekomaa kiumri na wana ufahamu mkubwa.

"Wanamuita Dennis kwa sababu watoto wangu saa hizi washakuwa wakubwa. Hawana zile pilka pilka za kuita mtu 'baba'," alisema.

Aliongeza "Walipokuwa wadogo ndio walikuwa wananisumbua wakiuliza kama wanaweza kuita mpenzi wangu 'baba."

Alisema kwa mzaha kuwa binti zake watatu kwa sasa wanapaswa kuwaita waume zao 'baba'.

Mama huyo wa watoto watano alisafiri kuelekea Ulaya takriban wiki moja iliyopita na aliweza kuzuru mataifa ya Uswizi na Ufaransa.

Wakati wa mahojiano, alibainisha kuwa sababu kuu ya ziara yake ilikuwa kununua mavazi yake muhimu yakiwemo gauni la harusi na chupi huku akiweka wazi kwamba huwa ananunua mavazi yake ya ndani nje ya nchi.

"Nilikuwa nimeenda kununua nguo zangu za ndani kwa sababu huwa sivai kutoka hapa Kenya kusema ukweli. Hizo ni vitu muhimu sana kuzingatia. Kubwa kabisa ni gauni langu la harusi kwa sababu nilitafuta nikakosa," alisema.

Ingawa watoto wake wawili wadogo wanaishi Ufaransa, mwimbaji huyo hakupata nafasi ya kuwatembelea wala kuwaona.

Alisema maandamano katika nchi hiyo ya Ulaya yaliathiri usafiri na hivyo hakuweza kufika katika eneo wanaloishi.

"Watoto wangu wanaishi mbali. Lazima ningechukua taxi kuenda Paris alafu tena nichukue treni kwa masaa manne. Wakati kuna mgomo kama huo, ni vigumu sana kufika kule. Kwa hivyo sijafika kule," alisema.

Mwanamuziki huyo hata hivyo alifichua kwamba aliweza kukutana na mchumba wake na kuwa na muda mzuri naye.