Mama unapoomba kuwa na mtoto kama Hakimi pia omba kuwa na mume kama huyo - Mr P

"Ukifurahi kijana yako kufanya jinsi Achraf Hakimi alifanya, pia tafakari itakuwaje kama mume wa binti yako atafanyiwa hivyo," - Msanii huyo wa PSquare alisema.

Muhtasari

•Msanii huyo wa PSquare alitoa maoni yake kuhusu Mchezaji Hakimi kumrithisha mama yake mali yote na si mke wake.

• Mke wa Hakimi alipigwa na butwaa baada ya kudai zaidi ya nusu ya urithi wa mumewe katika kesi ya talaka, lakini aliambiwa mali yote ya mumewe yapo chini ya jina la mamake.

Mr P amshtumu Hakimi kwa kuandikisha mali yake kwa jina la mamake.
Mr P amshtumu Hakimi kwa kuandikisha mali yake kwa jina la mamake.
Image: Instagram

Ijumaa kulikuwa na taarifa ambazo hazikudhibitishwa kwamab mchezaji wa kimataifa wa Morocco na timu ya PSG, Achraf Hakimi alikuwa amemrithisha mama yake mali yake yote.

Hili lilibainika baada ya mke wake raia wa Uhispania kupeleka kesi ya talaka mahakamani akidai Zaidi ya asilimia 50 ya mali ya beki huyo, lakini akapigwa na butwaa baada ya mahakama kubaini kwamba mchezaji huyo hakuwa na mali yoyote chini ya jina lake, bali mali yote yaliandikishwa kwa jina la mamake.

Kesi hiyo imekuwa gumzo la mitandao ya kijamii kwa siku tatu sasa, watu wakionekana kuwaganyika kwa makundi mawili.

Wapo wale waliomuunga mkono kwa kuwa mwerevu na kuweka mali yake kwa jina la mama yake – hawa wengi walikuwa watoto wa kiume.

Kwa upande mwingine, wanadada walimsuta mchezaji huyo kwa kuweka mali yote chini ya miliki ya mama yake hali ya kuwa alikuwa na mke, wakisema kuwa hakuwa anamuamini mke wake.

Ifahamike kuwa Hakimi ana miaka 24 tu huku mke wake akiwa na miaka 36, tofauti ya Zaidi ya miaka 12!

Msanii Peter Okoye anayefahamika Zaidi kwa jina Mr P kutoka kundi la PSquare ametoa maoni yake akisema kuwa Hakimi alimkosea heshima mke wake kwa kutomuandikishia mali yake.

Kulingana na Mr P, kina mama wote ambao wanamshangilia Hakimi kisa kamwandikishia mamake mali yake pia wanafaa kutafakari itakuwaje hali sawa na hiyo ikijitokeza kwa waume zao na wao wakiwaandikishia mama zao mali na si wao.

Aliwataka kina mama wanapoomba kuwa ni mtoto kama Hakimi wa kuwarithisha mali, pia waombe kuwa na mume kama huyo akifanya hivyo kwa mama yake, na pia mkwe kama huyo akifanya hivyo kwa mabinti zao.

“Huku kila mama akiomba kupata mtoto kama Achraf Hakimi, wasisahau pia kuomba kupata wanaume kama yeye na pia wakwe kama yeye,” Mr P alisema.

Alisisitiza kwamba si lazima kila mtu akubaliane naye na kusema kuwa kesi kama hiyo hukata pande zote mbili kama msumemo kwani wewe kama mama ukishabikia kijana yako kufanya hivyo, kumbuka pia na mume wa binti yako naye atamfanyia hivyo na utalihisi zito kama vile mama wa mke wa mtoto wako alihisi.