Tikiti za VVIP za tamasha la Boyz II Men zinazouzwa Ksh 30K kwa moja zimeuzwa zote!

Boyz II Men watatumbuiza kwa mara ya Kwanza Kenya kwa hisani ya Kampuni ya Radio Africa ikishirikiana na Benki ya Stanbic.

Muhtasari

• Tamasha la Stanbic Yetu Festival litafanyika mnamo Juni 10 jijini Nairobi na linaandaliwa na kampuni ya Radio Africa Group kwa ushirikiano na benki ya Stanbic.

• Tikiti za VVIP zilikuwa zinauzwa kwa shilingi elfu 30 kila moja na tayari zote zimeuzwa.

Tikiti za Stanbic Yetu Festival zimeuzwa zote kitengo cha VVIP.
Tikiti za Stanbic Yetu Festival zimeuzwa zote kitengo cha VVIP.
Image: RADIO JAMBO

Kamati andalizi ya tamasha kubwa kabisa la Stanbic Yetu Festival imetangaza kuwa tikiti za kiwango cha juu Zaidi, VVIP ambazo zilikuwa zinauzwa shilingi elfu 30 kila moja tayari zimeuzwa zote.

Tamasha la Stanbic Yetu Festival litafanyika mnamo Juni 10 jijini Nairobi na linaandaliwa na kampuni ya Radio Africa Group kwa ushirikiano na benki ya Stanbic.

Katika tamasha hilo, kundi maarufu la miziki ya RnB kutoka Marekani, Boyz II Men ndio watakuwa watumbuizaji wakuu wakialikwa jukwaani na wasanii ainati wa kutoka humu nchini.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Boyz II Men kutia maguu yao kwenye udongo wa Afrika, na ni bahati kubwa Zaidi kwamba Nairobi, Kenya itakuwa sehemu ya kupokea nyayo zao kwa mara ya kwanza na baadae waondoke kwenda nchini Uganda na Afrika Kusini mtawalia.

Kamati andalizi ilitangaza kwamba tiketi za rasha zinakwenda kwa shilingi elfu 8 kila moja huku zile za VIP zikiuzwa kwa shilingi elfu 15 kila moja na zile za VVIP ambazo zimeisha tayari zitauzwa kwa shilingi elfu 30 pesa taslimu kila moja.

Kikundi cha BoyzII Men kilifafanua upya muziki maarufu wa RnB na kinaendelea kuunda vibao vya kudumu vinavyovutia mashabiki kote na vizazi vyote.

Tuzo 4 za Grammy za kikundi hicho ni tone tu la ufuta katika bahari ya mafanikio yao. Katika taaluma yao ya miaka 25, Boyz II Men wameshinda tuzo tisa (9) za ajabu za Muziki za Marekani, Tuzo tisa (9) za Soul Train, tatu (3) Tuzo za Billboard, miongozi mwa tuzo zingine.

Tamasha hilo pia litashuhudia baadhi ya Dj bora wa Kenya akiwemo DJ G-Money, DJ Forro, Dj Shaky, DJ Grauchi, CNG na DJ Dream.

 

Kando na Muziki, tamasha hilo pia halitakamilika pasipo na vinywaji vya kujiburudisha. Mwaka huu Pernod Ricard Kenya watakuwepo kama wafadhili rasmi kwa upande wa utoaji.

 

Hoteli ya Sankara ni mshirika wa hoteli kwa mara nyingine kwa ajili ya Tamasha la Stanbic Yetu huku mshirika wa usafiri angani akiwa ni Kenya Airways.