Professor Jay apona kabisa na kupata hamu ya kula, ni 'Operesheni Rudisha Shavu'

Msanii huyo alipakia picha ya video akiwa anashambulia vyakula ainati kwa raha ya aina yake, akisema ni operesheni ya kurudisha mwili wake kama zamani maadamu amepata hamu ya kula.

Muhtasari

• Mashabiki na wafuasi wake walionesha furaha yao kumuona msanii huyo akifurahia chakula baada ya kulazwa kwa miezi kadhaa.

• Mwaka mmoja baadaye, Prof Jay amerejea akiwa na nguvu zaidi na kushiriki safari yake ya kupona na wafuasi wake wa mitandao ya kijamii.

Professor Jay atangaza operesheni ya kurudisha mwili baada ya vita dhidi ya ugonjwa kwa mwaka mmoja.
Professor Jay atangaza operesheni ya kurudisha mwili baada ya vita dhidi ya ugonjwa kwa mwaka mmoja.
Image: Instagram

Rapa wa muda mrefu katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva ambaye pia ni mwanasiasa Joseph Haule almaarufu kwa jina la kisanii kama Professor Jay amepakia habari njema kwa mashabiki na wafuasi wake, akionesha kujirudi kabisa katika hali yake ya kawaida.

Msanii huyo ambaye alifanya ujio mpya mitandaoni wiki chache zilizopita baada ya kupigana vita ya ugonjwa kwa Zaidi ya mwaka mmoja uliopita alitangaza kuwa hatimaye amepata hamu ya kula.

Jay alipakia video na picha akiwa anasasambua vyakula ainati kwenye Instagram yake na kusema kuwa maadamu amepata hamu ya kula na afya kujirudi, hana budi kupoteza muda bali ni kuanza mashambulizi ya vyakula ili kurudisha mwili wake, akiita ‘Operesheni ya kurudisha mashavu yake’.

Leo Nimeanza rasmi Oparation Rudisha Shavu, nikiwa na mdogo wangu wa damu,” Professor Jay aliandika kwenye picha hizo.

Katika video moja, wimbo wa kutia moyo na kurudisha shukrani kwa Mungu ulikuwa unacheza kwa mbali huku Jay na mdogo wake kila mmoja akichukua nafasi yake katika kuitendea haki meza ile iliyokuwa na vyakula vya kila rangi, herufi na aina.

Mashabiki wake pamoja na wasanii wenzake ambao wamekuwa wakisimama naye kwa muda mrefu kwa njia ya maombi walifurahi ajabu kumuona Jay amejirudi katika hali sawa na kumtaka azidishe juhudi za kurudisha shavu kwani chakula kilikuwa kimemkataa kwa miezi mingi.

“Ndugu yangu, hii ni nzuri sana kuona.. Mungu ni mkubwa, Alhamdulillah,” msanii mwenza, Mwana FA alimwambia.

“Mimi raha ninayoiskia kukuona unatabasamu tu,” msanii na mwigizaji Shilole alisema kwa furaha.

“Vizuri sana kukuona ukirudisha hadithi yetu inayoheshimiwa sana. Maoni yangu; Piga zoezi sana. Punguza nyama nyekundu na badilisha na nyeupe halafu zidisha matunda matunda na mboga @professorjaytz. Mapambano yanaendelea... 😊” mtangazaji wa redio kutoka Kenya Willy Tuva alimwandikia.

Jay alikuwa amelazwa hospitalini kwa miezi kadhaa, ikiwemo kulazwa katika chumba cha uangalizi maalum.

Mbunge huyo wa zamani pia alifanyiwa dialysis kwani figo zake pia ziliathirika.

Mwaka mmoja baadaye, Prof Jay amerejea akiwa na nguvu zaidi na kushiriki safari yake ya kupona na wafuasi wake wa mitandao ya kijamii.