Yesu wa Tongaren arudi darasani kupata mafunzo kuhusu Yesu wa kweli

Wachungaji kutoka Angaza Bible College walisema kuwa walivizia biblia ya Yesu wa Tongaren na wakaona ni ya Kweli na hivyo kumwalika kukubali ofa ya ufadhili.

Muhtasari

• "Njooni tusemezane. Si ni Baraka, wacha Kenya ibarikiwe na wachungaji wote wa Kenya,” alisema Yesu baada ya ziara hiyo nyumbani kwake.

Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Image: Maktaba

Ni afueni kwa Yesu wa Tongaren baada ya taasisi moja ya mafunzo ya kidini kaunti ya Bungoma kujitokeza na kumpa ufadhili wa kusomea theolojia – masomo ya Biblia.

Kulingana na taarifa katika runinga ya West TV, Kennedy Anaswa Musee ambaye ni naibu chansela wa taasisi hiyo ya Angaza alisema kiongozi huyo tata wa dini ana nafasi ya kujiunga kwa ufadhili huo ili kupanua upeo wa akili na mawazo Zaidi kuhusu injili.

Naibu chansela huyo alitaja umuhimu wa Yesu wa Tongaren kujiunga kwani utamwezesha kupata cheti na pia kuweza kulisajili kanisa lake kulingana na sheria za Kenya.

“Ameturuhusu tuione Biblia yake, pia tumemvizia na tumeona anatumia Biblia ya kawaida, tumemwambia ni busara mtumishi wa Mungu ajiunge na shule ya theolojia kwa sababu anahitaji cheti cha diploma ya theolojia na pia kuweza kulisajili kanisa lake hili hapa ambalo halijasajiliwa," Musee alisema.

Uongozi wa chuo hicho anuwai ulikinzana na taarifa zinazoenezwa kwamba Yesu wa Tongaren hadhamini elimu wakisema kuwa wakisema kuwa watoto wa mchungaji huyo wengi wako shuleni.

“Yesu wa Tongaren watoto wake wanasoma, mimi nafunza mtoto wake anaitwa Michael, na ni mtoto mzuri, mtiifu. Hata juzi amekuja  sababu ya karo kidogo, na tulikubali huyo mtoto asome,” mwalimu mmoja kutoka eneo hilo alisema.

Kwa upande wake, Yesu wa Tongaren aliwarai wachungaji wengine kutomuogopa na kuwapa karibu nyumbani kwake kwa ajili ya kusemezana.

“Wale ambao mlikuwa mnaniuliza maswali mbona wachungaji wananiogopa. Leo wamefika kunitembelea na tumesemezana sawa na maandiko ya Isaya 1:18 na wachungaji wengine mmekaribishwa. Njooni tusemezane. Si ni Baraka, wacha Kenya ibarikiwe na wachungaji wote wa Kenya,” alisema.

Baada ya kusemezana naye, wachungaji hao kutoka chuo anuwai cha Angaza Bible College walisema kuwa Yesu alikubaliana na ofa hiyo ya ufadhili wa theolojia.

Yesu wa Tongaren anapata ufahdili huu siku moja tu baada ya video kuibuka na mkewe akiwaomba wahisani wema haswa viongozi wa serikali kumpa Yesu zawadi ya gari ili kurahisisha safari za hapa na pale kueneza injili.