Eric Omondi na mpenziwe wanatarajia mtoto baada ya mimba ya kwanza kuharibika

“Imenichukua miaka 41 lakini hatimaye Mungu amenibariki na zangu kuona matunda ya viuno vyangu," - Omondi.

Muhtasari

• "Ninahisi kama Sara wa Abrahamu anayetajwa katika Biblia, alingoja maisha yake yote kupata mtoto wake mwenyewe,”

Eric Omondi atangaza ujauzito na mpenzi wake.
Eric Omondi atangaza ujauzito na mpenzi wake.
Image: Instagram

Mchekeshaji Eric Omondi na mpenzi wake wa muda mrefu Lynn wametangaza kutarajia mtoto wao wa kwanza miezi michache baada ya kutangaza kuharibikiwa na mimba yao ya kwanza.

Omondi kupitia ukurasa wake wa Instagram alipakia picha nzuri wakiwa na mpenzi wake wake lakini pia ishara ya ujauzito ulikuwa bayana kabisa kama meno ya ngiri.

Mchekeshaji huyo alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kuishi na hatimaye kukaribia kuona zao lake baada ya miaka 41 ya kutua duniani.

Omondi alijifananisha na hadithi ya Sarah na baba wa Imani Abraham kutoka Biblia ambao walilazimika kusubiri kwa miongo kadhaa kabla ya kupata mtoto wao wa kimiujiza, Isaka.

“Imenichukua miaka 41 lakini hatimaye Mungu amenibariki na zangu. Tunda la viuno vyangu. Ninahisi kama Sara wa Abrahamu anayetajwa katika Biblia, alingoja maisha yake yote kupata mtoto wake mwenyewe,” Omondi aliandika.

Pia mchekeshaji huyo ambaye pia ni mwanaharakati alimshukuru mpenzi wake kwa kuvumilia na kustahimili maumivu ya kuharibikiwa na mimba, na pia kumshukuru Mungu kwa kumfidia na mtoto mwingine baada ya mimba kuharibika.

“Asante mpenzi kwa kunifanya baba❤❤🙏🙏 . Na kwa Mungu asante kwa kuturudishia mtoto wetu,” Omondi alishukuru.

Mwaka jana, wawili hao walitangaza habari za kukata maini kwamba wameharibikiwa na mimba yao, japo baadhi ya watu hawakumchukulia kwa uhakika wakidhani kwamba alikuwa anafukuzia kiki kama ambavyo imekuwa kawaida yake kwa muda sasa.

Kando na mimba hiyo, pia itakumukwa wakati mmoja aligeuka gumzo baada ya kuonekana na msanii Miss P wakidanganya kuwa walikuwa kwenye mapenzi na hadi kuonesha picha za kile kilidhaniwa kuwa ni mimba lakini baadae ikabainika kwamba alikuwa anazua kiki baada ya kudai amempa mkataba katika lebo aliyoianzisha.

Kipindi hicho, Miss P alikuwa ameondoka kishari katika lebo ya msanii Willy Paul, Saldido.