"Ninaongoza wasanii, si madokta" - Kenzo ajibu wanaotilia shaka elimu yake kama rais wa wasanii UG

Eddy Kenzo alikiri kwamba elimu yake ni ya darasa la tatu lakini ueewa wake katika muziki ni wa juu mno katika utayarishaji, uandishi, uigizaji na uongozaji wa muziki.

Muhtasari

• Aliwaambia wakosoaji kwamba "karatasi (za masomo) sio muhimu sana" linapokuja suala la kuongoza kundi la wanamuziki.

Eddy Kenzo ajibu wanaokosoa elimu yake katika uongozi wa wasanii Uganda.
Eddy Kenzo ajibu wanaokosoa elimu yake katika uongozi wa wasanii Uganda.
Image: Instagram

Msanii Eddy Kenzo ambaye ni rais wa wasanii wa taifa la Uganda amevunja kimya chake baada ya kukejeliwa na kudhihakiwa mitandaoni kwamba hawezi kuwa rais hali ya kuwa hajasoma vizuri.

 Baada ya kuongoza mkutano wa kwanza wa wasanii wa Uganda, ambapo lilikuwa ni jukwaa linalotarajiwa kuwakutanisha wanamuziki kutoka vyama tofauti nchini Uganda, ili kujiinua zaidi na kuendeleza maslahi yao katika tasnia hiyo, ndani na nje ya nchi, kulikuwa na mashambulizi mabaya kutoka kwa pembe tofauti, kuhusu sifa zake za uongozi.

Kenzo hata hivyo aliwajibu wakosoaji wake akisema kuwa elimu si kigezo katika uongozi wa wasanii kwani yeye anachokijua ni kwamba anaongoza wasanii na wala si madaktari.

Akijibu, mwimbaji huyo aliyeteuliwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika tuzo za Grammy na ambaye anasema alisoma tu hadi darasa la 3, aliwaambia wakosoaji kwamba "karatasi (za masomo) sio muhimu sana" linapokuja suala la kuongoza kundi la wanamuziki.

Kilicho muhimu zaidi, alisema, ni uelewa wa kina wa tasnia, changamoto na fursa zake na uzoefu, ambao anao kwa wingi.

“Sitakuwa nikiongoza madaktari wakuu au walimu; Mimi ni kiongozi tu wa wanamuziki. Haiwezi kuwa kuhusu vitabu lakini kazi”, Kenzo alisema alipokuwa akionekana kwenye Galaxy FM ya nchini humo.

"Wale ambao wana wasiwasi wanapaswa kuzungumza juu ya kile ninachojua. Nina ufahamu sana linapokuja suala la sanaa na muziki; Mimi ni mtayarishaji, mwandishi, mwigizaji na mwongozaji,” alisema.

“Ninapoanza kuzungumzia muziki, huwezi kunitilia shaka. Mimi ni mtu ninayeweza kwenda kujaza viwanja katika nchi ambazo hata hawajui ninaimba nini. Kwa hivyo, nadhani ninaruhusiwa kuongoza shirikisho la wanamuziki.”

Kando na hilo, Kenzo anasema shirikisho lina sekretarieti ambayo itashughulikia mambo ya kiufundi na magumu, wakati "sisi wakubwa" tunasimamia.