Tiktoker Brian Chira akamatwa kwa madai ya kumchafulia Azziad jina

Wakati wa live yake, Chira alimtusi Azziad na kuenda kiwango cha kuwapea wafuasi wake namba ya simu ya Azziad.

Muhtasari

• Chira anadaiwa kutoa kauli za kashfa kuhusu Azziad wakati wa kipindi cha moja kwa moja kwenye Tiktok yake siku chache zilizopita. 

• Zaidi ya hayo, Chira alifichua bila kujali maelezo ya kibinafsi ya Azziad mtandaoni, na kumfanya apokee simu nyingi ambazo hazijaombwa na zinazosumbua kutoka kwa watu asiowajua.

Brian Chira akamatwa kwa madai ya kumchafulia jina Azziad
Brian Chira akamatwa kwa madai ya kumchafulia jina Azziad

TikToker maarufu Brian Chira, usiku wa kuamkia leo amekamatwa baada ya kushtakiwa na muunda maudhui Azziad Nasenya kwa madai ya kumchafulia jina. 

Chira alikamatwa nyumbani kwake katika kaunti ya Nakuru, kama ilivyothibitishwa na wakili wa Azziad, Getrude Kibare.

Chira anadaiwa kutoa kauli za kashfa kuhusu Azziad wakati wa kipindi cha moja kwa moja kwenye Tiktok yake siku chache zilizopita, na kumharibia jina jambo ambalo kulingana na wakili wake lilimsababishia dhiki kubwa.

Kulingana na Getrude Kibare, live ya Chira kwenye Tiktok ilikuwa na matamshi ya kuudhi yaliyomlenga Azziad, yakitumia lugha mbaya na ya kudhalilisha. Zaidi ya hayo, Chira alifichua bila kujali maelezo ya kibinafsi ya Azziad mtandaoni, na kumfanya apokee simu nyingi ambazo hazijaombwa na zinazosumbua kutoka kwa watu asiowajua.

Katika kukabiliana na kashfa na madhara yanayoweza kutokea kwa maisha ya kibinafsi na kitaaluma ya Azziad, aliamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Chira chini ya Sheria ya Uhalifu wa Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao.

Tukio hilo limeibua wasiwasi mitandaoni ya kijamii, kwani linaangazia umuhimu wa utumiaji wa uwajibikaji wa majukwaa ya mtandaoni na madhara yanayoweza kusababishwa na kueneza habari za uwongo.

Wakili wa Azziad, Getrude Kibare, alisisitiza kuwa watafuatilia kesi inayomkabili Chira mahakamani ili kutafuta haki kwa mteja wake.

Letu ni kukuhimiza wewe msomaji uweze kuwajibika na kujichunga wakati unatumia mitandao ya kijamii.