Natarajia rais Ruto kunitambua na kunipa zawadi - mpishi Maliha baada ya rekodi ya Guiness

Kwa mujibu wa Maliha, rais Ruto wakati anatunuku mwanariadha Faith Kipyegon kwa kuweka rekodi mpya kwenye riadha, alisema kuwa Mkenya yeyote atakayeweka au kuvunja rekodi atatuzwa.

Muhtasari

• Kwa kunyoosha rekodi, Maliha alisema hii sio mara ya kwanza kwake kuweka rekodi mpya.

• Akizungumza na Moses Sagwe, mwandishi wa Radio Jambo, Maliha Mohammed alisema kwamba anatarajia jawabu kutoka Guiness wiki hii.

Chef Maliha ategemea Ruto kumzawadi.
Chef Maliha ategemea Ruto kumzawadi.
Image: Instagram, Facebook

Mpishi Maliha Mohammed amevunja kimya chake ikiwa ni Zaidi ya wiki moja baada ya kuweka rekodi mpya ya dunia katika kitabu cha Guiness kwa kupika chakula ndani ya nyumba kwa Zaidi ya saa 90.

Mohammed licha ya kuvunja rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na mpishi Mmarekani Rickey Lumpkin wa California, aliyepata muda wa kupika nyumbani wa saa 68, dakika 30 na sekunde 1 Desemba 2018, ametuarifu kupitia mahojiano ya kipekee kwa njia ya simu kwamba Guiness bado hawajampa jawabu – ikiwa ni Zaidi ya wiki moja tangu kumaliza rasmi kupika.

Akizungumza na Moses Sagwe, mwandishi wa Radio Jambo, Maliha Mohammed alisema kwamba anatarajia jawabu kutoka Guiness wiki hii, akionesha matumaini makubwa kwamba jawabu hilo litakuwa chanya kwani alizingatia vigezo vyote vilivyotolewa na Guiness.

“Hii wiki ndio wanatupatia majibu, ninategemea majibu yatakuwa sawa sababu niliwatumia ushahidi wa kupika kwangu. Tunangoja,” Maliha alisema.

Maliha alisema kwamba pindi Guiness watakapotambua rekodi yake, anategemea kuwa kiongozi wa taifa Dkt William Ruto atamtambua na kumpa zawadi.

Kwa mujibu wa Maliha, rais Ruto wakati anatunuku mwanariadha Faith Kipyegon kwa kuweka rekodi mpya kwenye riadha, alisema kuwa Mkenya yeyote atakayeweka au kuvunja rekodi atatuzwa.

“Ninategema zawadi kutoka kwa rais wetu. Natarajia atanipa msaada wa kifedha. Bado hajatoa maoni yoyote lakini naamini ashafikishiwa ujumbe kupitia mitandao ya kijamii. Alisema ahadi yake kwamba anayevunja rekodi yoyote ya dunia atapewa zawadi na serikali,” Maliha alisema.

“Kuna watu wengi walikuja kuona na kila mtu alikuwa anajua kwa hiyo ujumbe amepatiwa. Ikitokea nimekutana na Ruto sasa hivi nitamuomba asaidie watu ambao wako na talanta zao zikuzwe na kuinuka. Katika sekta ya talanta changa. Kuna watu wako na talanta lakini labda kwa sababu ya mkwamo wa kihela hawaifanyii bidii. Kwa hiyo nitamuomba awape jukwaa la kujikuza Zaidi,” Maliha aliongeza.

Kwa kunyoosha rekodi, Maliha alisema hii sio mara ya kwanza kwake kuweka rekodi mpya akisema kwamba rekodi yake ya kwanza aliiweka mwaka 2019 ambayo ilikuja kuvunjwa baadae.