Obinna amkosoa Mulamwah kujenga nyumba kubwa ya kifahari kijijini

"Wakati mwingine kujenga kijijini ni uwekezaji mbaya. Kwa sababu muda mwingi haupo pale, unajenga nyumba unawekeza mamilioni Zaidi ya kumi na huishi pale,” Obinna alisema.

Muhtasari

• Mchekeshaji huyo hata hivyo alishauri kwamba hajasema watu wasijenge lakini anasema ikiwa unajenga, usiwekeze pesa nyingi hali ya kuwa mjini unateseka.

Obinna akosoa Mulamwah kujenga mjumba mkubwa Kijijini
Obinna akosoa Mulamwah kujenga mjumba mkubwa Kijijini
Image: Insta

Mchekeshaji na mkuza maudhui Oga Obinna amemkosoa vikali mchekeshaji mwenzake Mulamwah kwa kuwekeza hela zake nyingi katika ujenzi wa jumba la kifahari kijijini mwao hali ya kuwa jijini Nairobi anaishi katika nyumba ya kukodisha yenye chumba kimoja cha kulala.

Akizungumza na SPM Buzz, Obinna alisema kwamba kujenga kijijini hali ya kuwa muda wako mwingi unautumia mjini ni uwekezaji uliopotoka na mbaya.

Obinna alisema kwamba yeye ni mmoja wa wale wachekeshaji wa kwanza kujenga kijijini mwao lakini sasa hivi akirudisha muda nyuma anaona ni kama alikosea katika maamuzi ya kujenga kijijini.

“Mimi nilijenga kitambo, nafikiri mimi ndio wachekeshaji wa kwanza kujenga. Nilijengea wazazi wangu, nikajijengea lakini wakati mwingine kujenga kijijini ni uwekezaji mbaya. Kwa sababu muda mwingi haupo pale, unajenga nyumba unawekeza mamilioni Zaidi ya kumi na huishi pale,” Obinna alisema.

“Kama mimi nyumba yangu huwa nalala pale mara chache sana, nikienda Kisumu nalala kwa hoteli napitia nyumbani kidogo kuona kama nyasi zimekatwa. Nikienda nyumbani nalala pale kama usiku 2 tu na muda mwingi mimi niko Nairobi,” aliongeza.

Mchekeshaji huyo hata hivyo alishauri kwamba hajasema watu wasijenge lakini anasema ikiwa unajenga, usiwekeze pesa nyingi hali ya kuwa mjini unateseka.

“Sina maana kwamba watu wasijenge, jenga lakini usiwekeze pesa nyingi. Kama una pesa nyingi sawa, lakini kama huna jenga nyumba karibu na sehemu utakayoishi,” alisema.

Obinna alisema kwamba yeye anapanga kupata nyumba jijini Nairobi akiwa na bajeti ya milioni 30 lakini akasema akipata pesa nzuri atajenga au kununua nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 60.

Wikendi iliyopita, Mulamwah aliwaonesha mashabiki wake mjengo wa kifahari anaoujenga nyumbani kwao Kitale akisema kwamba mpaka kule ulikofikia kwa angalau asilimia 70, tayari ametumia Zaidi ya shilingi milioni kumi.

Mulamwah pia aliwaonesha mashabiki wake jinsi mjengo huo utakavyoonekana baada ya kukamilika.