Mama aliniunga mkono katika ndoto zangu za awali za kuwa padri - Wakili Kipkorir akumbuka

"Leo nimetafakari sana juu ya kifo cha Mama yangu mweiz Mei. Mama yangu bila elimu alinifundisha kuwa Mkatoliki wa Kirumi mwenye maombi…" alisema.

Muhtasari

• "Hata katika hali yake ya kiafya, mama yangu alichunguza afya yangu na kama nimekula. " Kipkorir alisema.

akimsafirisha mamake kwenda India mnamo Mei 19,2023.
Wakili Donald Kipkorir akimsafirisha mamake kwenda India mnamo Mei 19,2023.
Image: TWITTER// DONALD KIPKORIR

Wakili Donald Kipkorir amemkumbuka marehemu mama yake aliyefariki mwezi Mei mwaka huu kwa ujumbe wa kihisia.

Kupitia kurasa zake mitandaoni, wakili huyo maarufu aliibua kwamba marehemu mama yake alimfunza jinsi ya kuwa kijana wa kuomba sana.

Licha ya kwamba mama yake hakuwa mtu mwenye elimu, alimfunza kijana wake jinsi ya kukariri punje za tasbihi za kanisa Katoliki.

Wakili huyo pia alifichua kwamba mama yake alikuwa mtu wa kwanza kabisa kumuunga mkono katika ndoto yake ya awali ya kuwa padre wa kanisa Katoliki.

“Leo jioni, nilitafakari juu ya kifo cha Mama yangu Mpendwa, Katarina mwezi wa Mei baada ya kuugua saratani… Mama yangu bila elimu alinifundisha kuwa Mkatoliki wa Kirumi mwenye maombi… Aliniunga mkono katika ndoto zangu za awali za kuwa Padri…” Kipkorir alikumbuka kwa hisia za uchungu.

Alisema kuwa anapitimiza miezi mitatu tangu kifo cha mama, ni mtu ambaye alihakikisha kwamab amesoma katika shule nzuri zenye hadhi ya aina yake kijijini na kumtaka aendelee kupumzika mahala pema penye wema siku zote hadi siku ya kiyama.

“Lakini alihakikisha nimesoma shule bora zaidi ya msingi katika Mahali petu (sasa Kata) … Alinitakia mema zaidi … Hata katika hali yake ya kiafya, mama yangu alichunguza afya yangu na kama nimekula. Leo, nilitafuta upendo na baraka zake. Nimemkumbuka mama yangu,” Kipkorir alisema.

Mnamo mwezi Mei, Kipkorir alifichua kwa uchungu kwamba mama yake alifariki nchini India alikokuwa amemsafirisha kwa ajili ya matibabu ya saratani ambayo ilikuwa imemsumbua kwa muda mrefu.

"Nikiwa njiani kuelekea India na mama yangu. Mama yangu Kipenzi Katarina amepata maumivu makali sana. Nikiwaombea wataalam bora wa magonjwa ya saratani nchini India wampe mama yangu ahueni na uponyaji. Mbingu zitusikie," alisema.

Alikuwa akifanyiwa matibabu ya radiotherapy hapa nchini Kenya kabla ya kusafirishwa hadi India.