Harmonize yuko kwenye Beast Mode, atangaza kurekodi nyimbo 7 ndani ya saa 24

"Tunatengeneza EP ndogo ya magoma 7 tunaita 24 kwa sababu ngoma zote zitazalishwa ndani ya saa 24 kuanzia saa nne usiku wa leo Afrika Mashariki hadi kesho muda kama huu, utakutana na EP hiyo ipo tayari kabisa,” alisema.

Muhtasari

• Ikumbukwe siku si nyingi Harmonize alitangaza kwamba alikuwa katika safari ya kuachia albamu yenye ngoma nyingi za Kiingereza pekee.

Harmonize
Harmonize
Image: Insta

Harmonize katika siku za hivi karibuni amekuwa akionesha ufanisi mkubwa wa kilele katika muziki wake akiwa na kasi ya ajabu katika kuachia ngoma baada ya ngoma bila kupoa.

Msanii huyo baada ya kuachia nyimbo tatu kwa mpigo wiki chache zilizopita, sasa amerudi akitangaza nonda juu ya nonda kwa kutimba studioni na kurekodi magoma 7 kwa mfululizo na yote kutoka ndani ya saa 24 tu!

Kupitia Instagram story yake, Harmonize alipakia video ikimuonesha produsa wake wa muda mrefu B Boy akiwa ameketi kwenye studio akisanifu midundo na kusema kwamba walikuwa tayari kwa guu kukanyaga lami ndani ya saa 24 kuzalisha nyimbo 7.

“Katika muda wa miezi 7 sijapata kuonana na kaka yangu BBoybeats na sasa tumekutana leo, tunatengeneza EP ndogo ya magoma 7 tunaita 24 kwa sababu ngoma zote zitazalishwa ndani ya saa 24 kuanzia saa nne usiku wa leo Afrika Mashariki hadi kesho muda kama huu, utakutana na EP hiyo ipo tayari kabisa,” alisema.

Watu wengi wamekuwa wakisifia kile wazungu wanaita workrate yake katika siku za hivi karibuni.

Ikumbukwe siku si nyingi Harmonize alitangaza kwamba alikuwa katika safari ya kuachia albamu yenye ngoma nyingi za Kiingereza pekee kama njia moja ya kujiuza katika masoko ya kimataifa ya muziki.