Msanii Maua Sama azungumzia wakati mgumu alipompoteza mwanawe

“Nilipoteza mwanangu lakini sikupoteza Imani, Ukiona mtu amenenepa muache hujui nini anapitia nyuma ya Pazia,” Maua Sama aliandika.

Muhtasari

• Sama kwa huzuni alisema kwamba lilikuwa ni pigo ambalo halitokuja kusahaulika katika moyo wake.

Maua Sama
Maua Sama
Image: Insta

Mwaka wa 2022 haukuwa rahisi kwa msanii Maua Sama kutoka upande wa +255 Bongo.

Msanii huyo alipoteza mwanawe kwa maana ya kuharibikiwa na ujauzito na lilikuwa ni tukio kubwa sana ambalo liliwagusa watu wengi wakiwemo mashabiki na wasanii wenzake.

Ikiwa ni mwaka mmoja tangu kupatwa na hilo pigo, Maua Sama anaonekana bado anaendelea kuumia sana, kwani wenye midomo wanasema kuwa mzazi kumzika mwanawe ni sawa sawa na kuzika sehemu ya nafsi yake.

Katika kipindi hicho chote licha ya kuonekana akitoa ngoma za binafsi na kolabo lakini mtu mwenye umakini anaweza akaona msanii huyo hayupo sawa kabisa kwani amekuwa akichapisha vitu katika kurasa zake mitandaoni zikionesha mtu mwenye huzuni sana.

Siku tatu zilizopita Maua Sama aliachia wimbo wake kwa jina Kiss Me na katika moja ya chapisho la kuupigia promo kwenye ukurasa wake wa X, awali mtandao huo ukijulikana kama Twitter, alikumbuka tena kupoteza mwanawe.

Sama kwa huzuni alisema kwamba lilikuwa ni pigo ambalo halitokuja kusahaulika katika moyo wake lakini vile vile akakiri kwamba licha ya yote yaliyotokea, hakuwahi kupoteza Imani, huku akiwataka mashabiki wake kusimama upande wa faraja yake kwa kusapoti wimbo huo wake mpya.

“Nilipoteza mwanangu lakini sikupoteza Imani, Ukiona mtu amenenepa muache hujui nini anapitia nyuma ya Pazia,” Maua Sama aliandika.

Bila shaka jambo la kuharibika kwa mimba kwa mwanamke yeyote ni jambo lenye ukakasi mwingi wenye kuzua ukungu machoni mwake.

Wengine huathirika kisaikolojia kwa kiasi kwamba hata inafikia kipindi wanahitaji ushauri nasaha kutoka kwa wanasaikolojia.

Tunatumai Maua Sama ataweza kupata faraja katika moyo wake na kupata kifurushi kingine kama hicho kilichomtoka.