Inakuwaje wanasheria halali kushindwa na wakili bandia kwa kesi 26? - Ezekiel Mutua auliza

Inaarifiwa kwamba Mwenda alikuwa ameshiriki katika kesi nyingi kwenye mahakama mbali mbali na kushinda 26 kati yao mbele ya majaji na wanasheria waliohitimu kwa njia halali.

Muhtasari

• Mwenda kwa wakati mmoja aliwahi kumwakilisha aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga.

Ezekiel Mutua ashangazwa na uwezo wa wakili bandia Brian Mwenda.
Ezekiel Mutua ashangazwa na uwezo wa wakili bandia Brian Mwenda.
Image: Facebook

Mwenyekiti wa bodi inayosimamia hakimiliki za kazi za Sanaa humu nchini MCSK, Daktari Ezekiel Mutua amejiunga na Wakenya wengine wengi kujiuliza swali la kushangaza kuhusu wakili feki Brian Mwenda aliyekamatwa Alhamisi jijini Nairobi.

Mwenda alitiwa nguvuni na chama cha wanasheria wa Kenya, LSK tawi la Nairobi na inaarifiwa kwamba alikuwa ameshiriki kama mwanasheria wa mahakama ya juu kwa muda mrefu licha ya kuwa hajawahi tia guu lake katika darasa lolote la mafunzo ya uanasheria.

Baada ya kugundulika kwamba Mwenda alikuwa ameshinda kesi 26 katika kuwawakilisha wateja mbalimbali, Mutua alionesha kushangaa kwake kuhusu ushindi huo wake ambao ulitokea mbele ya majaji na wanasheria wengine wengi ambao wamehitimu kwa njia halali.

“Inakuwaje hadi wanasheria na mawakili waliohitimu halali kushindwa katika kesi si mara moja, bali mara 26 na wakili bandia?” Mutua aliuliza akiashiria kwamba hadithi nzima kuhusu ujasiri na kujitolea kwa aina yake kwa wakili bandia Brian Mwenda ni ya kushangaza.

Saa chache baada ya habari kusambaa kwamba Mwenda amekamatwa na kugundulika kuwa mwanasheria bandia, Wakenya walizama kwenye makabrasha na kuchimbua video akiwa mahakamani na jinsi alivyokuwa anawatatuiza wanasheria na majaji kwa maswali makali na umahiri katika kuwasilisha hoja zake.

Mwenda kwa wakati mmoja aliwahi kumwakilisha aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga ambaye amekuwa abururwa kuwa mgeni wa dola mahakamani mara kwa mara.

Mwenda hata hivyo alipata afueni baada ya muungano wa chama cha wafanyikazi nchini COTU kupitia kwa mwenyekiti wao Francis Atwoli kujitokeza na kumtetea akisema kuwa COTU watasimama naye.

Kupitia kwa waraka aliouchapisha kwenye Twitter, Atwoli alisema kwamab si jambo geni kwa mtu kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kitivo au Nyanja ambazo hawajazisomea na hivyo kueleza kwamba kuna haja ya kijana huyo kusaidiwa katika kupata mafunzo ya uanasheria badala ya kumkandamiza.