Koffi Olomide avunja kimya kurejea Kenya Desemba baada ya marufuku ya 2016

"Ninasema kwamba nitajaribu kuwa rafiki mzuri ambaye nilikuwa hapo awali,” Koffi Olomide aliambia watangazaji wa Radio Jambo.

Muhtasari

• Picha ya video ya tukio hilo inamuonyesha Olomide akimpiga teke na hata kumburuza mwanamke huyo ambaye inasemekana ni mmoja wa wacheza densi wake.

• Baadaye alikamatwa nje ya studio za Citizen TV na kufukuzwa hadi Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Koffi Olomide
Koffi Olomide
Image: Facebook

Wapenzi wa miziki ya Rhumba - yenye asili yake kutoka taifa la Kongo na ukanda wa Afrika ya Kati kwa jumla, mpo?

Msanii wa muda mrefu katika tasnia ya Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Koffi Olomide kwa jina la majazi kama Mopao Mokonzi atakuwepo nchini Kenya kuanzia tarehe 9 Desemba.

Olomide alithibitisha haya katika mahojiano ya pekee kwa njia ya simu na stesheni ya Radio Jambo, katika kipindi cha Asubuhi cha Gidi na Ghost.

Akizungumzia ujio wake baada ya Zaidi ya miaka 5 tangu kupigwa marufuku kutua nchini kufuatia tukio la kuzozana na shabiki wa kike mwezi Julai 2016, Mopao Mokonzi alisema kwamba amewamiss sana mashabiki wake aliowatambua kama ‘ndugu na dada zangu’ wa Kenya.

Msanii huyo pia alishukuru uongozi wa sasa ukiongozwa na rais Ruto kwa kurahisisha ujuo wake, ikiwa ni baada ya kupigwa marufuku kwake 2016.

“Ni ukweli ninakuja Kenya, na ujio wangu ni Desemba 9 jijini Nairobi. Ni shoo yangu ya kwanza baada ya kama miaka 6. Ningependa kusema ahsante kwa uongozi mpya wa Kenya ambao ni rais na ofisi yake na ningependa pia kuwaambia mashabiki wangu, ndugu zangu na dada zangu ninao Kenya ambao nimewamiss sana Kenya, ninasema kwamba nitajaribu kuwa rafiki mzuri ambaye nilikuwa hapo awali,” Koffi Olomide aliambia watangazaji wa Radio Jambo.

Mamlaka ya Kenya iliondoa marufuku iliyokuwa imezuia mwanamuziki huyo kuingia nchini humo kufuatia tukio la kushambuliwa ambalo lilizua taharuki Julai 2016.

Picha ya video ya tukio hilo inamuonyesha Olomide akimpiga teke na hata kumburuza mwanamke huyo ambaye inasemekana ni mmoja wa wacheza densi wake.

Baadaye alikamatwa nje ya studio za Citizen TV na kufukuzwa hadi Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Pia katika mahojiano hayo, alijutia kile ambacho alisema kilitokea 2016 na kusema kwamba alijihisi vibaya sana lakini hatimaye amekuwa huru na atajumuika na mashabiki wake Nairobi kwa mara nyingine.