Dvoice akikiuka mkataba wa Wcb Wasafi atatozwa faini bilioni 2 - Babake afichua (video)

"Kipengele kigumu, huyu bwana alikuwa kwanza anatakiwa asionekane katika kumbi za muziki alivyosajiliwa. Na akionekana analipa bilioni 2. " babake alisema.

Muhtasari

• Dvoice alisainiwa Novemba 16 na kuingia katika historia ya Wasafi kama msanii wa 7 kuandikishwa ndani ya lebo hiyo tangu Februari 2016.

Dvoice
Dvoice
Image: Screengrab

Wiki moja baada ya Dvoice kuingia katika mkataba na lebo ya muziki ya Wasafi kama kinda mpya wa kujaribu kuzivaa buti zilizoachwa na Rayvanny mwaka jana, sasa imeanza kubainika vipengele vigumu vya mkataba huo.

Baba mzazi wa Dvoice aliweza kufuatwa nyumbani kwake na waandishi wa habari za mitandaoni na kutoa mwanga kidogo katika baadhi ya vipengele ambavyo aliviona vigumu.

Ikumbukwe awali tuliripoti kwamba Baba Levo, chawa wa Diamond alifichua kwamba Dvoice alipewa mkataba muda mrefu akakaa chini na familia yake na kuvisoma vipengele vyote na wao kama lebo wanatumai kwamba hadi kufikia hatua ya kutia sahihi, maanake alikubaliana na vipengele hivyo.

Babake Dvoice alisema kwamba kipengele kimoja kilikuwa kinazungumzia adhabu mwanawe atakabidhiwa iwapo atakiuka masharti ya mkataba.

Alisema kwamba Dvoice pindi baada ya kutambulishwa, hafai kutangamana na watu wowote katika kumbi za starehe au kujiamulia kufanya shoo popote pasi na ufahamu wa Wasafi.

Endapo atakiuka kipengele hicho, basi atapigwa faini ya shilingi bilioji 2 za kitanzania, hela ambazo mzee baba alisema kwake ni vigumu na ndio maana alimuasa mwanawe kuzingatia masharti yote katika mkataba.

“Wasafi wana sheria kali, na kama huna Imani huwezi kusaini. Kwa sababu kwanza unapewa mkataba unausoma, kipengele kipi unachoona kigumu, unauliza na wenyewe wanakujibu palepale. Kipengele kigumu, huyu bwana alikuwa kwanza anatakiwa asionekane katika kumbi za muziki alivyosajiliwa. Na akionekana analipa bilioni 2. Sasa mimi ndani humu hata elfu 2 sina,” alisema mzee baba.

“Sasa hapo unakaa na mwanao unamwambia umeona jinsi mkataba ulivyokuwa mgumu huu, sasa ni ujiangalie. Na kweli yule bwana kadri tulivyowasiliana na kuonana, bwana sisi hali yetu duni na mikataba yao migumu bwana jiangalie mwanetu, sawa na yeye mwenyewe akawa mtiifu mpaka anakuja kutangazwa, hatujasikia suala la aina yoyote,” aliongeza.

Dvoice alisainiwa Novemba 16 na kuingia katika historia ya Wasafi kama msanii wa 7 kuandikishwa ndani ya lebo hiyo tangu Februari 2016.