Shughuli ya kumtambulisha Dvoice peke yake ilichukua zaidi ya milioni 100 - Baba Levo

"Kwa hiyo ikifika muda wa Diamond kuanza kuchukua hela yake na kuwekeza pale, hakuna muda wa kuanza kulalamika na kulia kwenye media machozi mengi."

Muhtasari

• "Kuanzia maandalizi ya ukumbi wenyewe, vitu vilivyowekwa mle, watu walioalikwa na vitu kama hivyo ni Zaidi ya milioni mia.”

Baba Levo na DVoice
Baba Levo na DVoice
Image: Instagram

Chawa na msiri mkubwa wa Diamond Platnumz na lebo nzima ya WCB Wasafi, Baba Levo amefichua kwamba utambulisho wa msanii mpya, Dvoice katika lebo hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita uligharimu kiasi kikubwa cha pesa.

Akizungumza katika kikao cha Friday Night kwenye runinga ya East Africa, Baba Levo alikanusha kwamab msanii huyo alishurutishwa kusaini mkataba kwa lengo la kusaidiwa.

Levo alisema kwamba alipewa mkataba na akakaa nao kwa muda wa kutosha kuuelewa katika kila kipengele kabla ya kuamua kwamba anataka kusainiwa na pia kutoa nafasi kwa mkurugenzi Diamond Platnumz kuanza kuwekeza kwake na mwisho wa siku mtu anahitaji marejesho ya faida kutokana na uwekezaji.

“Mkataba amepewa Dvoice kaka nao muda wa kutosha, kakaa na familia yake na wameusoma na kuuelewa, masharti na sheria zote amesoma na amekubaliana na kile kilichoandikwa mle ndani. Kwa hiyo ikifika muda wa Diamond kuanza kuchukua hela yake na kuwekeza pale, hakuna muda wa kuanza kulalamika na kulia kwenye media machozi mengi, ni kwamba unatakiwa uanze kurudisha hela ya watu kwa sababu watu wamewekeza fedha pale,” alisema.

Baba Levo hata hivyo alisema kwamba hiyo si njia moja ya kumsimanga msanii huyo wala kuhisi kwamba atafika kati kabla ya kukamilisha mkataba wake.

“Sio kwamba tunamsimanga lakini tunampa angalizo ili ajue na awe anapiga hesabu ya kila hela ambayo inawekwa. Angalia utambulisho wake tu peke yake tulitumia Zaidi ya milioni 100. Kuanzia maandalizi ya ukumbi wenyewe, vitu vilivyowekwa mle, watu walioalikwa na vitu kama hivyo ni Zaidi ya milioni mia.”