Jinsi Khaligraph alimvulia kofia Musalia Mudavadi na kumuamrisha 'panda juu ya steji'

Kwa wakati mmoja alimuuliza Mudavadi kama angetaka kuchukua kipaza sauti ili kuwaimbia mashabiki lakini waziri huyo kwa tabasamu na kucheka akasema hawezi.

Muhtasari

• Musalia Mudavadi na mwenzake wakajongea jukwaani wakiwa wamevalia vilemba vya ‘father christmas’.

Khaligraph Jones na Musalia Mudavadi.
Khaligraph Jones na Musalia Mudavadi.
Image: Screengrab

Wikendi iliyopita msanii Khaligraph Jones alikuwa na nafasi adimu ya kutumbuiza kwenye tamasha la uzinduzi wa Cocacola Caravan kwa ajili ya msimu wa Krismasi ambapo miongoni mwa wageni waalikuwa alikuwa mkuu wa mawaziri ambaye pia ni waziri wa masuala ya nje, Musalia Mudavadi.

Kile kilichowachekesha mashabiki wake ni jinsi alivyomkaribisha Mudavadi na wanasiasa wenzake jukwaani.

Khaligraph alianza kwa kuvua kofia yake na kudai kwamba hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa kupata nafasi ya kualika wanasiasa jukwaani lakini akasema atajaribu lakini kwa jinsi alivyojaribu ndio aliwaacha hoi wengi.

“Mpaka nimetoa kofia, samahani waheshimiwa, sijawahi fanya hili kabla, sijui jinsi ya kualika wanasiasa jukwaani. Lakini nitajaribu kufanya vizuri jinsi nijuavyo. Tafadhali, panda juu ya steji,” OG aliongea kwa sauti ya kutoa amri.

Musalia Mudavadi na mwenzake wakajongea jukwaani wakiwa wamevalia vilemba vya ‘father christmas’ kabla ya Khaligraph kuanza kuimba nao wimbo wa ‘Sifu Bwana’ – kolabo ya nguvu aliyomshirikisha Nyashinski mwaka mmoja uliopita na ikafanya vizuri ajabu.

Kwa wakati mmoja alimuuliza Mudavadi kama angetaka kuchukua kipaza sauti ili kuwaimbia mashabiki lakini waziri huyo kwa tabasamu na kucheka akasema hawezi.