Solomon Mukubwa afichua siri ya kukatwa mkono wake katika mazingira yenye utata

"“Nikafanya miaka 3 naweka mkono kwa maji ya dawa, mfupa ulikuwa unaonekana mweupe. Miaka 3 mkono unaoza, ulikuwa ukija kunitazama ukirudi unalia." alisema.

Muhtasari

• “Hii ni mwezi mmoja baada ya kuzika mdogo wangu aliyeharisha kwa siku mbili tu na kufa." Mukubwa alisema.

Solomon Mukubwa
Solomon Mukubwa
Image: Screengrab

Msanii wa injili kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC ambaye makazi yake ni nchini Kenya, Solomon Mukubwa amesimulia kwa kirefu mazingira yenye utata yaliyopelekea kukatwa kwake mkono wa kushoto.

Msanii huyo alifanya kikao na runinga ya Global TV Online nchini Tanzania ambaye alidokeza kwamba kulikuwepo na mchango mkubwa wa nguvu za giza uliochangia kukatwa kwa mkono wake baada ya kuteseka kwa Zaidi ya miaka 3 na usaha.

Hitmaker huyo wa Mfalme wa Amani alifichua kwamba zogo lote lilianza pale babake katika ziara yake ya ulevi alipatana na mwanamke mwingine kisha wakashiriki mapenzi lakini baada ya mwanamke huyo kupata mimba babake akaikataa hadi walipozaliwa mapacha na mmoja akafa.

“Baba aliikataa ile mimba na mpaka mapacha kuzaliwa bado aliwakataa watoto. Pacha mmoja akafa ikaletwa bili ya hospitali lakini tena baba akaikataa. Kwenye mazishi, babu ya yule pacha akaongea akasema ‘mjukuu wangu ulikataliwa na baba kutoka siku ya kwanza, lakini nakuhakikishia hautaenda mwenyewe’. Walipofanya mambo yao taarifa zikatufikia sisi tukajua kama ni vita tutapigana ngumi tu,” Mukubwa alisema.

Kwa kuashiria kwamba maneno ya yule mzee yalikuwa ya semi za kichawi, baada ya wiki moja tu dadake Solomon Mukubwa naye akaharisha siku mbili tu na kufa, akiwa mtoto wa miaka 4.

Kutoka hapo msururu wa majanga yakawa yanaiandama familia yake akisema kwamba walikuwa wamepuuzilia yale maneno ya yule mzee kwamba ‘mjukuu wangu hautaenda peke yako’.

Naye akiwa kidato cha tatu akitoka shuleni na wenzake, wakicheza barabarani akaangushwa lakini kufika nyumbani akasikia mkono wake umesinyaa. Mama akampa huduma ya kwanza lakini kesho yake hakuweza kuamka.

Na hivyo ndivyo safari ya kukatwa kwa mkono wake ilianza pasi na kujua.

“Hii ni mwezi mmoja baada ya kuzika mdogo wangu aliyeharisha kwa siku mbili tu na kufa. Tulienda hospitali wakanipitisha kwa scan wakidhani nimevunjika, scan ikaonesha mkono uko sawa. Kumbe ni kazi ya shetani. Ikafika hatua tukaenda kufanyiwa upasuaji, daktari kuliko apasue mahali Fulani, akapasua mkono mpaka akakata mishipa yote…”

“Nikafanya miaka 3 naweka mkono kwa maji ya dawa, mfupa ulikuwa unaonekana mweupe. Miaka 3 mkono unaoza, ulikuwa ukija kunitazama ukirudi unalia. Ilibidi madaktari kutoka Uswizi wakasema mkono umeharibika na wakaamua suluhisho ni kukatwa mkono, nilikuwa na miaka kama 14,” alisema.

Lakini hapo mzunguko mwingine wa maisha ulikuwa umeanza, Mukubwa alisema alifika mahali akaanza kujihisi ananyanyapaliwa na hata kufikiria kujitoa uhai.

“Nikaanza kuimba na watu wakawa wananiletea pes asana, sasa shetani akaja na kunisuka akili akaniambia ni kama naonewa huruma. Na mimi nikitoka hapo napatwa na hasira naambiwa Mungu kama nilikatwa mkono ili watu wanionee huruma, mimi nitakusaidia nijiuwe, nilianza kuwa na vita na nafsi yangu nikitaka kujiua,” alisema.