Huku akipanga kuwafukuza wanawe nyumbani kwake, tazama mambo yanayomfanya Zari mzazi wa kipekee

Hivi majuzi, Zari alidokeza kuwafukuza wanawe wakubwa kutoka nyumbani kwake akisema kuwa tayari wamekuwa watu wazima.

Muhtasari

•Zari alisema wanawe ni watu wazima ambao wanafaa kuanza kujitafutia maisha na sio tu kuendelea kulelewa na mama yao wakati wameshazidi miaka 18.

•Baada ya kutengana na marehemu Semwanga takriban miaka minane iliyopita, Zari amekuwa kwa mahusiano mengine zaidi ya tano na kwa kawaida huwa hawafichi wapenzi wake.

Mwanasoshalaiti Zari Hassan pamoja na watoto wake watano
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Hivi majuzi, mjasiriamali maarufu wa Uganda mwenye makaazi yake Afrika Kusini, Zari Hassan alifichua mipango ya kuwafukuza vijana wake watatu aliozaa na marehemu Ivan Ssemwanga kutoka nyumbani kwake ili kwenda nje kujitafutia maisha yao.

Zari alifichua mipango hiyo katika klipu ya TikTok akihojiwa ambapo alisema kwamba kwa sasa wanawe hao ni watu wazima ambao wanafaa kuanza kujitafutia maisha na sio tu kuendelea kulelewa na mama yao wakati wameshazidi miaka 18.

Zari alisema kwamba kinachomchochea Zaidi kuwafukuza nyumbani kwake ni baada ya klipu ya hivi majuzi ambayo iliwaonesha wakipigania nafasi ya kuegesha magari, kila mmoja akitaka kuliegesha gari lake kwenye nafasi moja.

"Bado tunapigana kuhusu maegesho katika yadi yangu, lakini natumai, wavulana wangu watahama mwaka ujao. Wanamiliki vyumba na magari, na wanahitaji kwenda. Wanahitaji tu kwenda. Kwa hivyo tunatumai kuwa hilo litapangwa mwaka ujao," alisema.

Zari amekuwa akiishi vizuri na watoto wake watano nchini Afrika Kusini na amekuwa kielelezo halisi cha uzazi wa kisasa ambapo watoto wako huru sana na wazazi wao na wanaruhusiwa kufanya wanavyotaka na kufanya maamuzi yao wenyewe.

Miezi michache iliyopita , mwanasholaiti huyo alionekana akiburudika katika eneo la burudani pamoja na wanawe wawili wakubwa Pinto Tale na Raphael Ssemwanga Jr

Kwenye Instagram, mama huyo wa watoto watano alionyesha video na picha zake na wanawe katika kilabu cha kifahari ambapo walionekana wakifurahia wakati mzuri.

Katika video hizo, watatu hao ambao pia walikuwa pamoja na marafiki wengine wa wanawe Zari walionekana kuwa na furaha nyingi na tabasamu ambazo zilijaa nyusoni mwao zilidhihirisha hilo

Katika video moja,  Zari alionekana akibugia glasi ya mvinyo huku mwanawe mkubwa, Pinto Tale akirekodi matukio hayo ya kufurahisha kwa kutumia kamera ya simu. Video nyingine ilimuonyesha Raphael akivuta moshi wa shisha huku mama yake akiwa amemshika kwenye bega.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Zari kuonekana na wanawe klabuni hapo, katika siku za nyuma aliwahi kuandamana nao kwenda kujiburudisha kwenye vilabu mbalimbali na kisha kurekodi matukio hayo kwenye mitandao ya kijamii.

Mwaka jana, mwanasoshalaiti huyo pia alionyesha picha na video zake na wanawe wakiburudika pamoja katika kilabu.

Kuburudika pamoja na wanawe ni moja tu ya viashirio vingi vinavyoonyesha mwanasoshalaiti huyo ana uhusiano wa karibu sana na watoto wake.

Mzazi kujivinjari pamoja na watoto wake bila kuzingatia pengo kubwa kati ta umri wake na wao sio jambo la kawaida hasa barani Afrika.

Zari akijivinjari na wanawe.
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Kando na hilo, Zari ameonekana kuwa tofauti sana na wazazi wengi wa Kiafrika kuhusu jinsi ya kusimamia mali na biashara za familia.

Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 43 amewaaminia  kwa kiwango kikubwa wanawe wakubwa  na usimamizi wa biashara  na mali  nyingi iliyoachwa nyuma na aliyekuwa mumewe marehemu Ivan Semwanga.

Mapema mwaka jana, Zari alianzisha mchakato wa kuhamisha uongozi wa Chuo cha Brooklyn City kwa watoto wake.

Mwezi Januari mwaka jana, mzaliwa huyo wa Uganda alitumia mtandao wa Instagram kutangaza kuwa amemteua mwanawe mkubwa Pinto Ntale kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Chuo hicho.

"Mkurugenzi Mtendaji Mkuu. mafunzo, wafundishe wangali vijana, siwezi kusubiri kumwona akichukua kampuni na kusimamia fedha,” Zari alisema.

Lingine linalomtofautisha Zari na wazazi wengine ni jinsi anaendeleza ushirikiano mzuri katika malezi na mzazi mwenzake Diamond Platnumz.

Wawili hao walitengana mwaka wa 2018 lakini hilo halijawazuia kushirikiana vizuri kuwalea watoto wao Tiffah Dangote na Prince Nillan.

Ushirikiano wa Diamond na Zari ni tofauti na jinsi anavyoshirikiana na wazazi wenzake wengine. Hii ni ishara kuwa mwanasoshalaiti huyo ana sifa ya kipekee ambayo huenda wapenzi wengine wa zamani wa staa huyo wa Bongo hawana

Kiashiria kingine cha jinsi mwasosholaiti huyo anaendeleza familia yake tofauti  njia za kitamaduni za Kiafrika ni jinsi ambavyo jinsi huwa haoni ugumu kutambulisha wapenzi wapya maishani mwake.

Kina mama wengi wa Kiafrika wameshindwa kujaribu mahusiano mapya baada ya kufiwa na waume zao au ndoa zao kuvunjika kwa kuhofia jinsi jamii na familia itawachukulia.

Baada ya kutengana na marehemu Semwanga takriban miaka minane iliyopita, Zari amekuwa kwa mahusiano mengine zaidi ya tano na kwa kawaida huwa hawafichi wapenzi wake.

Hata hivyo mahusiano yake hayajaonekana kuingilia uhusiano wake na wanawe. Wanawake wengi hawajaweza kufahamu siri ya kuruka kutoka kwa uhusiano mmoja hadi mwingine bila watoto wao kuathirika.

Zari pia ameweza kuwatambulisha watoto wake katika mitandao ya kijamii huku akiwafungulia akaunti za mitandao mbalimbali ya kijamii wakiwa wangali wadogo. Kando na kuwafungulia akaunti, pia ameweza kuwafundisha jinsi ya kutumia majukwaa hayo na jinsi ya kutengeneza maudhui yanayostahiki.

Hii ni mojawapo ya njia maalum za kuwatengenezea watoto hao wake maisha ya usoni kwani kadri akaunti zao zinavyoendelea kupata umaarufu ndivyo wataweza kuvuna umaarufu na kipato kutoka hapo.

Haya ni baadhi tu ya mambo yanayoonyesha kuwa mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz sio mzazi wa kawaida tu bali ni mzazi wa kipekee wa kisasa ambaye ameangazia kuwalea watoto wake tofauti na wengi.