Pasta Kanyari afichua kumtia kichapo jamaa aliyevunja TV yake, 'niijifaya namuondoa mapepo'

"Walipigana na mkewe wakavunja runinga yangu, nilikasirika lakini nikajua nikimchapa atapiga kelele watu wajae, kwa hiyo nikasema acha nijifanye namuombea nikimtoa makofi kumbe ni kumchapa."

Muhtasari

• Kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu na hakuwa anataka kuonekana kama anamuadhibu mwanamume yule, alimdanganya kwamba anataka kumuombea.

Pastor Kanyari
Pastor Kanyari

Mchungaji mwenye utata Victor Kanyari amekiri kwamba wakati mmoja alilazimika kujificha ndani ya maombi ya kuondoa pepo katika muumini mmoja kama njia ya kumuadhibu kwa kuvunja runinga katika studio yake.

Katika video ambayo imeenezwa kwenye mtandao wa TikTok, Kanyari anaonekana akihubiri na kufichua kwamba aliwahi patana na wanandoa wawili ambao hawakuwa na makaazi ya kulala.

Kwa kuwaonesha utu, Kanyari aliwaalika kwake na kuwapa chumba cha studio kukifanya kama makaazi yao lakini asubuhi moja alipata wamevunja runinga yake.

Kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu na hakuwa anataka kuonekana kama anamuadhibu mwanamume yule, alimdanganya kwamba anataka kumuombea kwa kumfukuzia mapepo, kumbe ndio alikuwa anatumia njia hiyo kumpa kichapo cha adhabu ya kuvunja runinga yake.

"Nilikuwa na TV kwenye studio yangu, nikawapa chumba cha kukaa, walipigana na kuvunja TV yangu. Nilikasirika sana nikataka kumpiga, lakini nilijua atapiga kelele na kuvutia majirani. Nilijifanya kama namuombea na kumtoa mapepo ndiyo maana unaona nampiga na kupiga kelele, watu walidhani ana mapepo kumbe hana, alivunja TV yangu tu," Kanyari alisema.

Video hii ya mchungaji huyo mtata inaibuliwa na Watumizi wa TikTok wakati ambapo kifo cha dadake mikononi mwa jamaa anayetajwa kuwa muuaji na tapeli wa kimapenzi kinaendelea kuwagawanya Wakenya mitandaoni.

Starlet Wahu alipatikana amefariki kwa kuchomwa kisu katika chumba cha AirBnB mtaani South B mwishoni mwa wiki iliyopita na kuzikwa Jumamosi alasiri katika hafla ya kifamilia.