"Watu wenye hela huwa hawajionyeshi" Stevo amjibu KRG kumuita kilema

“KRG afanye mambo yake na mimi nifanye mambo yangu, ila tu mimi nimemzidi kiumaarufu, kimziki, na kwa kila kitu. Ngoma za KRG hazina vina wala lolote." Stevo alisema.

Muhtasari

• Stevo alisema kwamba watu wenye pesa huwa hawajigambi lakini kwa KRG ni tofauti kwani hupenda kujigamba sana jinsi alivyo na hela ndefu.

• Msanii huyo alizidi kumtania akisema kwamba pesa anazodai kuwa nazo ni zake yeye [ Stevo] na kumtaka kumkabidhi.

Stevo na KRG
Stevo na KRG
Image: Facebook

Ugomvi baina ya wasanii KRG the Don na Stevo Simple Boy hauonekani kupata mwafaka wakati wowote hivi karibuni.

Hii ni baada ya wawili hao kila mmoja kumjibu kivyake mwenzake katika mahojiano mbalimbali, na majibu yao kwa kila mmoja ni ya shombo na ukakasi mkubwa.

Baada ya KRG kutokea kwenye kituo kimoja cha redio na kudai kwamba hana muda wa kujibizana na Stevo na kumkandia kuwa ni kilema, Rapa huyo wa kutoka Kibera naye amechaji betri yake na kumnyooshea KRG mtutu.

Katika mazungumzo na YouTuber, Trudy Kitui, Stevo alimshambulia KRG kuwa huenda hana pesa kama ambavyo amekuwa akijigamba mitandaoni.

Stevo alisema kwamba watu wenye pesa huwa hawajigambi lakini kwa KRG ni tofauti kwani hupenda kujigamba sana jinsi alivyo na hela ndefu.

Msanii huyo alizidi kumtania akisema kwamba pesa anazodai kuwa nazo ni zake yeye [ Stevo] na kumtaka kumkabidhi.

“Kwanza watu wenye pesa huwa hawajionyeshi, wanakaa kimya, kwa hiyo KRG anajionyesha anataka sifa. Na hizo hela ako nazo ni zangu, naomba tu anirudishie hela zangu,” Stevo alisema katika kile kilionekana kama ni utani.

"KRG wacha sifa na kiburi, fanya mambo yako na watu watakuelewa. Si eti mara uko huku na huku kama mbwa koko. Tafadhali fanya mambo yako na mimi nifanye ya kwangu," Stevo aliongeza.

Akijibu kauli ya KRG kuwa yeye ni kilemba ambaye hawezi jibizana naye, Stevo alimtaja msanii huyo kama mmbea na ambaye hafai kupewa nafasi yoyote kwenye vyombo vya habari kuzungumza.

“KRG amekuwa kama pikipiki posta kupayuka tu na maneno na wanahabari wameamua kumpa kipofu zawadi ya runinga. Si yeye mwenyewe aliniita kilema, kwa hivyo yeye pia ni kipofu. Mashabiki wangu mkilinganisha ngoma zangu na zangu, za nani zina maana? Zangu ama zake?” Stevo aliuliza.

Stevo alimtaka KRG kufanya mambo yake na kumwacha yeye ajishughulishe na ya kwake kwani hakuna penye wanaweza kutana, akisema kwamba kila mmoja anafanya kitu tofauti na mwenzake.

“KRG afanye mambo yake na mimi nifanye mambo yangu, ila tu mimi nimemzidi kiumaarufu, kimziki, na kwa kila kitu. Ngoma za KRG hazina vina wala lolote. Ukitaka kuona ngoma za maana ni zile zinaelimisha kila rika kutoka kwa watoto hadi kwa watu wazima, lakini za KRG hazina mafunzo kabisa,” Stevo alisema.