Dvoice afichua hisia zake kufananishwa na Rema kutoka Nigeria, kutamani kolabo

Dvoice alisema kwamba bosi wake – Diamond – ni staa duniani kwa hiyo kufanikisha kolabo yake na Rema itakuwa ni kupigiwa simu moja tu na kila kitu shwari.

Muhtasari

• Msanii huyo wa Singeli pia hakuweza kufutilia mbali uwezekano wa kufanya kolabo na mkali huyo wa Nigeria.

DVOICE NA REMA
DVOICE NA REMA
Image: Instagram

Msanii mpya wa Diamond Platnumz, Dvoice kwa mara ya kwanza ameweka hisia zake bayana baada ya kuona mitandaoni watu wakimfananisha na mkali wa Afrobeats kutoka Nigeria, Rema.

Mwezi Novemba mwaka jana alipotambulishwa rasmi kama msanii wa lebo ya WCB Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz, baadhi ya watu mitandaoni hawakuchelewa kumfananisha na Rema, si tu kwa tungo za miziki bali kwa muonekano wao ulioshabihiana kutoka kwa rangi ya ngozi hadi mtindo wa nywele.

Akilizungumzia hilo katika mahojiano na Wasafi FM, Dvoice alisema kwamba kama mtu mwingine yeyote yule, alifurahi kufananishwa na Rema kwani msanii huyo wa Nigeria ni mtu ambaye anafanya vizuri na kufananishwa na mtu ambaye anafanya vizuri katika kile anachokifanya ni heri na faraja kubwa.

“Hicho ni kitu kizuri tu kwa sababu nina Imani kwamba hakuna ubaya kufananishwa na mtu ambaye anafanya vizuri. Halafu pia Rema ukiangalia sio chizi wala bubu kiasi kwamba ningekuwa nasema kwamba dah, nimefananishwa na mtu Fulani ambaye labda ni mtu wa mabangi,” Dvoice alidhihirisha hisia zake.

“Ukiangalia nashukuru Mwenyezi Mungu Rema pale sioni kama ni kitu kibaya, naamini ni kitu kizuri kufananishwa naye na hiyo inatengeneza kitu Fulani kwamba kuna thamani ya mtu Fulani ambaye inawezekana ukakuja kuwa nayo baada ya miaka kadhaa, mtu anaweza akawa kama huyo mtu,” aliongeza.

Msanii huyo wa Singeli pia hakuweza kufutilia mbali uwezekano wa kufanya kolabo na mkali huyo wa Nigeria.

Dvoice alisema kwamba bosi wake – Diamond – ni staa duniani kwa hiyo kufanikisha kolabo yake na Rema itakuwa ni kupigiwa simu moja tu na kila kitu shwari.

“Natamani kufanya kazi na msanii yeyote ambaye anafanya vizuri Afrika. Nimeandaa ngoma nyingi tu lakini bado sijaweza kumfikia Rema kwa kolabo, kwa hiyo ni ndoto yangu tu hiyo. Uzuri wetu tajiri wetu ni staa duniani kwa hiyo tunachokifanya ni kupeleka ngoma na kumuuliza unatusaidiaje tukampata mtu Fulani,” alisema.